17. Hadiyth “Wanyama wanne hawafai kuchinjwa kwa ajili ya Udhhiyah… ”

al-Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisimama mbele yetu ambapo akasema: “Wanyama wanne hawafai kuchinjwa kwa ajili ya Udhhiyah… ” Imekuja katika riwaya nyingine: ”… hawatoshelezi; kipofu ambaye upofu wake unaonekana wazi, mgonjwa ambaye ugonjwa wake unaonekana wazi, kilema ambaye kilema chake ni cha wazi na dhaifu ambaye hana uboho.” [1]

Ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na wengineo. at-Tirmidhiy amesema: ”Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh.”

Hii Hadiyth ni dalili kuwa kasoro hizi nne haziwezi kukubaliwa katika mnyama wa Udhhiyah na mfano wake ni kila kasoro inayofanana nazo au kali zaidi.

1 – Kipofu wa wazi ni yule ambaye jicho lake limezama au limetoka nje. Ikiwa kuna doa jeupe tu kwenye jicho na halijasababisha upofu, inasihi kumchinja kwa Udhhiyah kwa kuwa upofu si wa wazi. Mnyama ambaye ni kipofu anaingia ndani ya hukumu hii kwa uzito zaidi. Hasihi hata kama jicho lake halikuzama, kwa sababu hawezi kutembea pamoja na kundi wala kula pamoja na wenzake.

2 – Mgonjwa wa wazi ni yule ambaye ugonjwa umeonekana wazi kwake kiasi kwamba hawezi kula vizuri au kuchunga na husababisha udhaifu mkubwa. Miongoni mwa mfano wake ni jirabu linaloonekana wazi, kwa kuwa huharibu nyama na mafuta.

3 – Kilema wa wazi ni yule ambaye ana kilema kinachoonekana. Kwa maana nyingine kutoweza kutumia mkono au mguu wake – ni mamoja iwe kwa sababu ya kuzaliwa hivyo au kwa ugonjwa wa baadaye. Na kilema wa wazi ni yule ambaye anaachwa nyuma na kundi kwa sababu ya kilema chake. Pia mnyama asiyeweza kutembea kwa sababu ya ulemavu anaingia ndani ya hukumu hii, kwa sababu hali yake ni mbaya zaidi kuliko kilema wa kawaida. Vilevile mnyama aliyevunjiwa mkono au mguu mmoja pia haifai kwa sababu amepungukiwa kiungo muhimu.

4 – Dhaifu ambaye hana uboho. Kwa maana nyingine mnyama ambaye hana ute wa ndani wa mifupa kwa sababu ya udhaifu uliopindukia. Lakini ikiwa kasoro ni ndogo haisababishi kutofaa, mfano ikiwa kuna doa dogo tu jichoni au kilema kidogo kisichomsababisha kuachwa nyuma na kundi, basi inasihi kumchinja. Hali kadhalika mnyama aliye na udhaifu usio wa kupindukia pia anafaa kwa Udhhiyah.

Hadiyth hii inafahamisha kwa maana pana kuwa kila kasoro iliyo nje ya hizi nne au isiyofanana nazo, haizuii Udhhiyah kuwa sahihi. Hii ni kwa sababu Hadiyth ilitolewa kwa lengo la kufafanua na kuweka mipaka, kwani ilikuwa ni jibu la swali. Dhahiri ni kwamba ilikuwa katika Khutbah ya hadhara kwa sababu al-Baraa´ ameleeza:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisimama mbele yetu… ”

Na kama kungekuwepo kasoro nyingine zinazozuia Udhhiyah ingelazimika kutajwa, kwa sababu kuchelewesha ufafanuzi wakati wa haja haifai.

Haitadhuru ikiwa mnyama amechomwa alama, masikio yake yamepasuliwa au kuchanwa au pembe yake imevunjika, kwa sababu mambo haya hayapunguzi nyama yake. Isitoshe jengine ni kwamba ni mambo yanayopatikana sana. Hata hivyo bora zaidi ni mnyama asiye na mambo hayo. Aidha haijuzu kuchinja Udhhiyah mnyama asiye na mkia – ikiwa ni kwa kukatwa – haifai kwa kuwa mkia ni kiungo muhimu. Lakini ikiwa mnyama hana mkia kwa uumbaji wake wa asili, basi inasihi kumchinja kwa Udhhiyah.

[1] Abu Daawuud (7/505), at-Tirmidhiy (5/81), an-Nasaa’iy (7/214) na wengineo.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 27-29
  • Imechapishwa: 13/05/2025