Tambueni – Allaah aniwafikishe mimi na nyinyi – ya kwamba swawm ya Ramadhaan ni miongoni mwa faradhi kubwa zaidi katika Uislamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ

“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga…”

mpaka aliposema:

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba kwa mwenye kuweza.”[2]

Kwa hiyo Aayah Tukufu inajulisha kwamba swawm ni faradhi. Hadiyth inafahamisha kwamba ni miongoni mwa nguzo za Uislamu.

Waislamu wameafikiana kwa maafikiano ya yakini juu ya uwajibu wa swawm ya Ramadhaan. Kwa hiyo yeyote atakayekataa uwajibu wake ni mwenye kuritadi kutoka katika dini ya Uislamu. Ataombwa atubie, akitubia sawa, na asipotubia atauawa. Kufunga Ramadhaan inawajibika juu ya kila muislamu. Yeyote atakayesilimu katikati ya mwezi atafunga kilichobaki tu. Halazimiki kulipa yaliyopita mwanzo wa mwezi.

Swawm inawajibika juu ya aliyebaleghe. Kuhusu mtoto mwenye utambuzi haimwajibikii swawm, lakini inasihi kwake kama swawm inayopendeza. Inatakikana kwa mlezi wake amwamrishe ikiwa anaweza ili aizoee na akue juu yake.

Swawm haimwajibikii mwendawazimu mpaka apate fahamu. Hilo ni kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kalamu imenyanyuliwa kwa watu watatu.”

Miongoni mwao ni:

“… mwendawazimu mpaka apate fahamu.”[3]

Kwa hivyo swawm inawajibika juu ya muislamu aliyebaleghe. Ikiwa ni mwenye afya na mkazi, basi inamlazimu kuitekeleza kwa wakati wake. Ikiwa ni mgonjwa, basi inamlazimu kuilipa baadaye. Vivyo hivyo mwanamke mwenye hedhi na mwenye damu ya uzazi inawalazimu kulipa swawm. Ikiwa ni mwenye afya lakini msafiri, basi amepewa chaguo kati ya kufunga kwa utekelezaji au kufungua na kulipa baadaye.

Yeyote katikati ya mchana atakuwa ni mwenye kustahiki uwajibu wa swawm, kama mfano wa kafiri aliyesilimu, mtoto akabaleghe, mwenye hedhi au damu ya uzazi akasafika, mgonjwa akapona, msafiri akarejea, mwendawazimu akapata fahamu au ushahidi ukasimama wa kuingia kwa mwezi katikati ya mchana, basi kila mmoja kati yao analazimika kujizuia sehemu iliyobaki ya mchana na watalipa siku hiyo. Hii ni kwa sababu ni siku ya Ramadhaan ambayo hawakufunga swawm sahihi na kamilifu. Hivyo ikawalazimu kuilipa. Wamelazimishwa kujizuia sehemu iliyobaki ya mchana kwa ajili ya heshima ya wakati.

[1] 02:185

[2] al-Bukhaariy (08) na Muslim (16).

[3] Abu Daawuud (4398), Ibn Maajah (2041), an-Nasaa’iy (3432), Ahmad (01/100) na al-Haakim (02/59) ambaye amesema:

”Ni Swahiyh juu ya masharti ya Muslim na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 05/02/2026