Kuna Bid´ah nyingi sana. Watu huzua Bid´ah nyingi. Bid´ah hazikubaliwi na wala hazitendewi kabisa, pasi na kuangalia ni zepi au zimetoka kwa nani. Miongoni mwa Bid´ah ni yale yanayofanywa katika kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Jambo hilo ni Bid´ah. Ni kitu kisichokuwa na dalili kutoka ndani ya Qur-aan, Sunnah wala mwongozo wa makhaliyfah waongofu. Hakuna karne yoyote katika zile karne zilizosifiwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa ni bora ilisherehekea. Ni jambo lilizuliwa baada ya karne hizi wakati ujinga ulipoenea. Wa kwanza waliozua mazazi ni Faatwimiyyah. Baada ya hapo yakachukuliwa na wazembe wanaojinasibisha na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wakadai kuwa wanasherehekea mazazi kwa nia njema na eti kwa ajili ya kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kusherehekea mazazi hakuhusiani kitu na kumpenda (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika si vyenginevyo mapenzi ya kweli ni kwa kumfuata, na si kwa kuzua:

Unamuasi Mungu na unadai kumpenda

Naapa kwamba kipimo hicho ni kibaya

Lau mapenzi yako yangelikuwa ya kweli ungelimfuata

Hakika mpenzi kwa ampendaye ni mwenye kumtii

Alama ya mapenzi ya kweli ni kwa kufuata. Uzushi ni alama ya kuchukia. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha Bid´ah ilihali wewe unazihuisha na kuzizua. Hiyo maana yake ni kuwa unachukia Sunnah. Ikiwa unachukia Sunnah basi unamchukia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ikiwa kweli unataka kheri, basi tubu kwa Allaah na urudi kwa Allaah. Ama ukaidi na kiburi yanakudhuru wewe mwenyewe.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 175-176
  • Imechapishwa: 02/12/2024