Shaykh Bakr amesema:

“Wacha tuseme kuwa maneno yake kweli yana ibara zisizokuwa wazi na zisizofungamana. Ni vipi mtu anaweza kuyafanya yakawa ni makosa ya kikafiri na kubomoa yote ambayo Sayyid Qutwub (Rahimahu Allaah) amejenga maisha yake juu yake kwa vile alilingania katika Tawhiyd ya Allaah katika hukumu na uwekaji wa Shari´ah na akatupilia mbali sheria za wanaadamu zilizotungwa na akakabiliana na wale wenye kuhukumu kwazo? Hakika Allaah anapenda uadilifu na inswafu katika kila kitu. Sikuonelei isipokuwa – Allaah akitaka – utarejea katika uadilifu na inswafu.”

Umeona wazi wazi kuwa namkufurisha Sayyid Qutwub katika vitabu viwili nilivyoandika juu yake mpaka ushtuwe namna hii? Unafikiria kuwa mimi ni kama Sayyid Qutwub na Qutbiyyuun wanaokufurisha watu na makundi kwa kuachia bila ya kuchunga masharti saba ya Salaf ya kukufurisha na moja wapo ikiwa ni kumbainishia haki yule mpinzani? Hukuona namna nilivyokuwa mkali kwake kumkemea juu ya Takfiyr yake kwa Ummah kwa sababu ya uongozi na si kwa sababu ya shirki kubwa wala mambo mengine ambayo wanachuoni wanakufurisha kwayo? Nilimkemea juu ya hilo kwa kurasa thelathini na tisa na sehemu nyingine takriban kurasa kumi na sita juu ya maasi makubwa na madogo ambayo yeye na ndugu yake na wafuasi wake wanaita kuwa ni “shirki”.

Unayafumbia macho makosa haya makubwa na ujinga na dhuluma iliyopindukia kwa waislamu na unaanza kusisimka na kupigwa na bumbuwazi kwa ajili ya kumuokoa Sayyid Qutwub? Hutikiswi na mshipa kabisa kwa makosa yake makubwa na makosa ya wafuasi wake.

Nimemfanyia vibaya na kumzulia uongo? Unajua namna anavyolingania katika Tawhiyd ya Allaah? Umesoma suala hili kwa umakinifu na utulivu? Sidhani kama umefanya hivo. Nafikiri tu kuwa umesikia maneno kutoka kwa wafuasi wake waliyopindukia na kisha ukapenda kuyakariri. Haya yanatiliwa nguvu na kule kukubali kwako mwenyewe ya kwamba hujasoma vitabu vya Sayyid Qutwub. Ungelisoma vitabu vyake kama Salafiy basi ungelikuta yafuatayo:

1- Tafsiri yake ya Qur-aan ni moja katika upotoshaji wake mbaya sana wa Aayah za Tawhiyd. Humo anafasiri Tawhiyd ya ´ibaadah kwenda katika Tawhiyd ya hukumu, uwekaji Shari´ah, siasa na uola. Kwa njia hiyo anaenda kinyume na maimamu wanaojulikana katika tafsiri ya Qur-aan. Uhakika wa mambo tafsiri yake si jengine isipokuwa ni tafsiri iliyopinda ya kisiasa.

2- Mbali na upotoshaji wake wa Tawhiyd mtu anapata kuona namna anavyofasiri Aayah za Tawhiyd kwa mfumo wa Khawaarij uliyopindukia unaokufurisha kwa njia ya kutokuchunga.

Hivi kweli ni kasoro na khatari ngapi zinazopatikana kwenye tafsiri yake ya Qur-aan? Hivyo basi, mche Allaah na usiwadanganye vijana.