Wanazuoni (Rahimahumu Allaah) wamekhitilafiana kuhusu mtu aliyekula au kunywa hali ya kuwa amesahau na yeye ni mwenye kufunga juu ya mitazamo miwili tofauti:

1 – Halazimiki kulipa siku nyingine na swawm yake ni sahihi. Haya ndio madhehebu ya wanazuoni wengi katika Hanafiyyah[1], Shaafi’iyyah[2] na Hanaabilah[3], ambayo ndio maoni sahihi ambayo wanaonelea hivo kikosi kikubwa cha wanafunzi wa Maswahabah, maimamu, wanazuoni na wakaguzi[4].

2 – Anapaswa kulipa siku hiyo aliyokula. Haya ndio madhehebu ya Imaam Maalik[5] na Rabiy’ah bin ´Abdir-Rahmaan[6] (Rahimahumu Allaah). Huenda Imaam Maalik hakufikiwa na Hadiyth na hivyo hakuipokea katika ”al-Muwattwa’”. Kwa hiyo anakuwa ni mwenye kupewa udhuru.

Sahihi ni kama ilivyotangulia ya kwamba hatoilipa siku hiyo, jambo ambalo linathibitishwa na Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (´Azza wa Jall) anasema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume.”[7]

Hoja ipo katika maneno ya Allaah na maneno ya Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Tazama ”al-Uswl-ul-Ma´ruuf bil-Mabsuutw” (02/201)  ya ash-Shaybaaniy  na ”al-Hujjah ´alaa Ahl-il-Madiynah  (01/391).

[2] Tazama ”al-Umm” cha ash-Shaafi’iy (02/106) na ”al-Haawiy al-Kabiyr” (03/456).

[3] Tazama ”Masaa-il Imaam Ahmad wa Ishaaq Ibn Raahuuyah (03/1236) na al-Mughniy (03/131) ya Ibn Qudaamah.

[4] al-Istidhkaar (03/319) cha Ibn ´Abd-il-Barr.

[5] ”al-Muwattwa´”  Malik (03/437) na ”al-Istidhkaar” (03/319) cha Ibn ´Abd-il-Barr.

[6] al-Istidhkaar (03/319) cha Ibn ´Abd-il-Barr.

[7] 04:59

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr Dhil-In´am bisharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/444)
  • Imechapishwa: 02/03/2025