16. Kusihi kutia nia mchana katika swawm ya kujitolea

Kuhusu swawm ya kujitolea, basi inasihi kwa nia ya mchana. Hilo ni kwa sharti kwamba kati ya kuchomoza kwa alfajiri na wakati wa nia hakujapatikana jambo linalobatilisha swawm kama kula na mfano wake. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kwangu siku moja akasema: ”Je, mna kitu chochote?” Tukasema: ”Hapana.” Ndipo akasema: ”Basi mimi ni mfungaji.”[1]

Hivyo kuomba kwake chakula kunathibitisha kwamba hakuwa amenuia kufunga kabla ya hapo. Maneno yake:

“Basi mimi nimefunga.”

yanafahamisha juu ya kuanza kwa nia mchana. Kwa hiyo ni jambo linafahamisha usahihi wa nia ya swawm inayopendeza kuanzia mchana. Basi hilo linakuwa ni jambo maalum kutokana na Hadiyth inayosema:

“Yeyote asiyelaza [nia ya] swawm kabla ya kuchomoza kwa alfajiri basi hana swawm.”[2]

Vilevile Hadiyth nyingine zilizo katika maana yake; kwamba hilo ni mahsusi kwa swawm ya faradhi na si zile za kujiolea. Hilo ni kwa sharti kwamba asitende kabla ya nia jambo linalobatilisha swawm kwa kuishia vile inavyopelekea dalili. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuhusu funga ya sunnah inatosha kutia nia sehemu ya mchana, kama yalivyofahamisha maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

‘Basi mimi nimefunga.”

´Ibaadah za kujitolea ni pana zaidi kuliko ´ibaadah za faradhi, kama vile swalah ya faradhi inavyowajibika ndani yake nguzo kama kusimama na kutulia juu ya ardhi, tofauti na swalah ya kujitolea kwani inasihi juu ya kipando na kwa anayetembea. Hiyo ni upanuzi kutoka kwa Allaah kwa waja Wake katika njia za kujitolea. Kwa sababu aina za ´ibaadah za kujitolea siku zote ni pana zaidi kuliko aina za ´ibaadah za faradhi. Haya ndio maoni ya kati na kati.”

Usahihi wa kutia nia ya swawm ya kujitolea kuanzia mchana ni jambo limepokelewa kutoka kwa jopo la Maswahabah ikiwa ni pamoja na Mu´aadh, Ibn Mas´uud na Hudhayfah. Aidha ni jambo lilifanyiwa kazi Abu Twalhah, Abu Hurayrah, Ibn ´Abbaas na wengineo.” Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] Wameipokea wanazuoni isipokuwa al-Bukhaariy. Ameipokea Muslim (1154).

[2] ad-Daaraqutwniy (02/172) na al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (04/202) ambaye amesema:

”Cheni yake ya wapokezi wote ni wenye kuaminika.”

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 05/02/2026