60 – Ahmad bin Naswr al-Khuzaa´iy (d. 231) – shahidi

220 – Imesihi ya kwamba Ibraahiym al-Harbiy ameeleza:

”Wakati Ahmad bin Naswr ameulizwa kuhusu ujuzi wa Allaah, akasema: ”Ujuzi wa Allaah uko nasi na Yeye yuko juu ya ´Arshi Yake.” Akaulizwa kuhusu Qur-aan ambapo akasema: ”Ni maneno ya Allaah.” Akaulizwa kama ni kiumbe ambapo akajibu: ”Hapana.”

61 – Mke wa Makkiy

221- Ahmad bin ´Aliy al-Abaar amesema: Muhammad bin ´Abdir-Rahmaan al-Balkhiy[1] ametuhadithia, Makkiy bin Ibraahiym amesema:

”Mke wa Jahm aliingia kwa mke wangu na akasema: ”Ee mama Ibraahiym, huyu ndiye mumeo anayezungumza kuhusu ´Arshi? Nani aliyeichonga?” Akajibu: ”Yule ambaye ameyachonga meno yako.”

Alikuwa na meno yaliyojitokeza kwa nje.

62 – Qutaybah bin Sa´iyd (150-240), shaykh wa Khuraasaan

222 – Abu Ahmad al-Haakim na mfasiri wa Qur-aan Abu Bakr an-Naqqaash, ambaye tamko ni lake, amesema: Abul-´Abbaas as-Sarraaj ametuhadithia: Nimemsikia Qutaybah bin Sa´iyd amesema:

”Hii ndio ´Aqiydah ya maimamu wa Uislamu na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah: Tunamjua Mola wetu yuko juu ya mbingu ya saba juu ya ´Arshi Yake. Kama alivosema (´Azza wa Jall):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[2]

Vivyo hivyo ndivo Muusa bin Harun alivyonukuu kutoka kwa Qutaybah, ambaye amesema:

” Tunamjua Mola wetu kuwa juu ya mbingu ya saba na juu ya ´Arshi Yake.”

Huyu hapa Qutaybah, ambaye anatambulika kwa uongozi na uaminifu wake, ambaye amenukuu maafikiano juu ya suala hili. Alikutana na Maalik, al-Layth, Hammaad bin Zayd na wakubwa wengine. Alikaa kwa muda mrefu na wanahifadhi wa Hadiyth walikuwa wakijazana kwenye mlango wake. Alimwambia mtu mmoja:

”Kaa nasi msimu huu wa baridi mpaka nikutolee kutoka kwa watu watano Hadiyth laki moja.”

Alifariki mwaka wa 240.

[1] Hivyo ndivyo ilivyoandikwa katika nakala zilizochapishwa na maandiko ya mkono. Naona kuwa ni kosa. Sahihi ni Muhammad bin ´Amr al-Balkhiy, kwani wamemtaja katika wapokezi wa Makkiy bin Ibraahiym. Naye ni Abu ´Abdillaah Muhammad bin ´Amr al-Balkhiy as-Swawwaaq ambaye ni mwenye kuaminika katika waalimu wa wa al-Bukhaariy, kama ilivyo kwa Makkiy bin Ibraahiym.  al-Abaar ni mwaminifu pia, mwenye kuhifadhi na madhubuti, kama alivosema al-Khatwiyb (4/306).

[2] 20:5

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Uluww lil-´Aliy al-Ghaffaar, uk. 173-174
  • Imechapishwa: 19/01/2026
  • Taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy