Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

124 – Tunaona kufaa kuswali nyuma ya kila mwema na muovu katika wale wanaoswali kuelekea Qiblah.

MAELEZO

Hapa kuna mambo mawili:

1 – Swalah ni kitendo chema. Wale wanaoswali, na khaswa ikiwa ni watawala, hakika wamefanya kitendo chema. Kuacha kuswali nyuma yao kunapelekea katika madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na uasi, kufarikisha umoja na umwagikaji wa damu. Hii ni dhambi kubwa, kwa msemo mwingine, ni kitu kisichotakiwa kupatikana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalini nyuma ya mwenye kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`, na kwa yule mwenye kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`.”[1]

Hapa ni kwa njia ya ujumla; tusemeje kuhusu kuswali nyuma ya watawala? Kuwatupilia mbali na kuasi kunapelekea uasi, kuleta mpasuko na mambo mengine mabaya yanayowapata waislamu.

Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah; wanaswali swalah ya ijumaa na swalah za mkusanyiko na wanapambana katika njia ya Allaah wakiwa bega kwa bega na kila kiongozi, ni mamoja ni mwema au muovu muda wa kuwa hajatoka nje ya Uislamu. Huu ni msingi moja wapo katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kuanzia zama za Maswahabah. Waislamu katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameafikiana juu ya jambo hilo.

[1]ad-Daaraqutwniy (1743).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 161-162
  • Imechapishwa: 25/11/2024