Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

أَيُشْرِكُونَ مَا لَا يَخْلُقُ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ وَلَا يَسْتَطِيعُونَ لَهُمْ نَصْرًا وَلَا أَنفُسَهُمْ يَنصُرُونَ

”Je, wanawashirikisha wale ambao hawaumbi kitu, na hali wao wenyewe wameumbwa, na wala hawawezi kuwanusuru na wala hawawezi kujinusuru nafsi zao?” (al-A´raaf 07:191-192)

2-

وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ

“Na wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki japo kijiwavu cha kokwa ya tende.” (Faatwir 35:13-14)

3- Imesihi kupokelewa kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipasuliwa siku ya Uhud na yakavunjwa meno yake mane. Akasema:

“Vipi watafaulu watu ambao wamempasua Mtume wao?”

Ndipo kukateremshwa:

لَيْسَ لَكَ مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ

”Si juu yako katika amri kuamua lolote.”[1] (Aal ´Imraan 03:128)

4- Imepokelewa kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba amemsikia Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema wakati akiinua kichwa chake kutoka katika Rukuu´ katika Rak´ah ya mwisho ya Fajr:

“Ee Allaah! Mlaani fulani na fulani!”

Haya aliyasema baad ya kusema:

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi. Mola wetu! Sifa zote njema ni Zako.”

Ndipo Allaah akateremsha:

لَيْسَ لَكَ مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ

”Si juu yako katika amri kuamua lolote.”[2] (Aal ´Imraan 03:128)

Katika upokezi mwingine imekuja ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba dhidi ya Swafwaan bin Umayyah, Suhayl bin ´Amr na al-Haarith bin Hishaam.” Ndipo kukateremka:

لَيْسَ لَكَ مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ

”Si juu yako katika amri kuamua lolote.”[3] (Aal ´Imraan 03:128)

5- Imesihi kupokelewa kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Alisimama Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipoteremshiwa:

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ

“Na waonye jamaa zako wa karibu.” (ash-Shu´raa 26:214)

na akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Enyi Quraysh – au maneno mfano wa haya – Zinunueni nafsi zenu! Hakika sintokufaeni mbele ya Allaah na chochote. Ee ´Abbaas bin ´Abdil-Muttwalib! Sitokufaa mbele ya Allaah na chochote! Ee Swafiyyah, shangazi yake Mtume wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Sitokufaa mbele ya Allaah na chochote. Ee Faatwimah, binti ya Muhammad! Niombe chochote katika mali yangu utakacho. Sitokufaa mbele ya Allaah na chochote.”

MAELEZO

1-

أَيُشْرِكُونَ مَا لَا يَخْلُقُ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ وَلَا يَسْتَطِيعُونَ لَهُمْ نَصْرًا وَلَا أَنفُسَهُمْ يَنصُرُونَ

”Je, wanawashirikisha wale ambao hawaumbi kitu, na hali wao wenyewe wameumbwa, na wala hawawezi kuwanusuru na wala hawawezi kujinusuru nafsi zao?”

Anachokusudia mtunzi kwa mlango huu ni kubainisha yale waliyokuwemo washirikina katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipowalingania na kuwapiga vita. Anabainisha ubatilifu wa hali zao inapokuja katika kumuabudu mwingine asiyekuwa Allaah walio na sifa hii. Mtu aliye na sifa kama hii hastahiki kuabudiwa. Swali limeulizwa kwa lengo la kuwakemea. Wao hawawezi kuumba hata nzi. Bali wao wenyewe wameumbwa. Ni vipi basi watawanufaisha wengine wasiokuwa wao? Wao ima ni viumbe visivyokuwa na uhai na visivyokuwa na akili au viumbe vilivyo hai lakini hawasikii au wafu wasiowatikia wale wenye kuwaomba. Katika Aayah wamesifiwa wale wanaowabudiwa badala ya Allaah kwa njia nne:

1-  Hawaumbi kitu.

2- Wao wenyewe wameumbwa na wanaendeshwa.

3- Hawawezi kuwanusuru.

4- Wao wenyewe hawawezi kujinusuru.

2-

وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ

“Na wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki japo kijiwavu cha kokwa ya tende.”

Allaah amewasifu waungu wao kwa sifa nne:

1- Hawamiliki chochote japo kijiwavu cha kokwa ya tende.

2- Hawasikii maombi ya wale wenye kuwaomba.

3-Hata kama watasikia hawatoweza kuwajibu.

4- Siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wa watu hawa. Hii ndio hali ya washirikina. Hakika wamekhasirika duniani na Aakhirah.

 3- Imesihi kupokelewa kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipasuliwa siku ya Uhud na yakavunjwa meno yake mane. Akasema:

“Vipi watafaulu watu ambao wamempasua Mtume wao?”

Ndipo kukateremshwa:

لَيْسَ لَكَ مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ

”Si juu yako katika amri kuamua lolote.”

Ikiwa kiumbe huyu mbora na Mtume ndiye ana manzilah ya karibu zaidi kwa Allaah hawezi kuitetea nafsi yake mwenyewe wala Maswahabah zake ambao ndio watu wa karne bora kabisa, basi ni dalili inayofahamisha kwamba hastahiki kuabudiwa badala ya Allaah wala kushirikishwa pamoja Naye. Yale yaliyomtokea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake kwa sababu ya dhambi zao yalitokea kwa sababu ya hekima kubwa. Ni vipi Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake, seuze wengine, wataombwa ikiwa wao wenyewe hawakuweza kujitetea nafsi zao wenyewe? Dhambi waliofanya ni kwenda kinyume na maamrisho ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale alipowaamrisha wapiganaji juu ya mlima kubaki katika nafasi zao.

4- Imepokelewa kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba amemsikia Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema wakati akiinua kichwa chake kutoka katika Rukuu´ katika Rak´ah ya mwisho ya Fajr:

“Ee Allaah! Mlaani fulani na fulani!”

Haya aliyasema baad ya kusema:

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi. Mola wetu! Sifa zote njema ni Zako.”

Ndipo Allaah akateremsha:

لَيْسَ لَكَ مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ

”Si juu yako katika amri kuamua lolote.”

Aliomba dhidi ya al-Haarith bin Hishaam, Swafwaan bin Umayyah na viongozi wengine wa Quraysh. Baada ya hapo wakaingia katika Uislamu. Allaah aliwaongoza na hakuitikia du´aa na laana dhidi yao. Ikiwa kiongozi na bwana wa wanaadamu hakukubaliwa du´aa yake na du´aa yake haikuwadhuru, vipi kuhusu wengine? Allaah ni mjuzi zaidi juu ya hali za waja Wake.

5- Imesihi kupokelewa kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Alisimama Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipoteremshiwa:

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ

“Na waonye jamaa zako wa karibu.”

na akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Enyi Quraysh – au maneno mfano wa haya – Zinunueni nafsi zenu! Hakika sintokufaeni mbele ya Allaah na chochote. Ee ´Abbaas bin ´Abdil-Muttwalib! Sitokufaa mbele ya Allaah na chochote! Ee Swafiyyah, shangazi yake Mtume wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Sitokufaa mbele ya Allaah na chochote. Ee Faatwimah, binti ya Muhammad! Niombe chochote katika mali yangu utakacho. Sitokufaa mbele ya Allaah na chochote.”

Amewakanushia kuwa udugu wao hautowafaa kitu ikiwa hatowamini. Amewaamrisha kuamini na kufuata yale aliyokuja nayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akawabainishia Tawhiyd na kwamba ndio njia ya uokozi. Tawhiyd ndio itakayowafanya kufaulu. Ama kuhusu mali yake, anaweza akawafaa nayo. Hili linatufahamisha kwamba ´ibaadah anastahiki kufanyiwa Allaah (Ta´ala) pekee na si mwingine. Ikiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawezi kumnufaisha yeyote mbele ya Allaah basi wengine wote wana haki zaidi ya kutoweza kufanya hivo.

Katika haya kuna Radd kwa washirikina ambao wanaomba manufaa kwa wengine asiyekuwa Allaah na huku wanasema:

مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah karibu” (az-Zumar 39:03)

Allaah ameita kitendo chao hichi kuwa ni shirki na akamwamrisha Mtume Wake kuwapiga vita kwa sababu walikuwa washirikina.

Kuhusu kumuomba kitu ambaye yuhai na muweza ni sawa. Ni miongoni mwa sababu zenye kuhisiwa na zenye kuingia akilini na hazina mahusiano yoyote na mambo yaliyofichikana wala wafu.

[1] al-Bukhaariy na Muslim (1791).

[2] al-Bukhaariy (4070).

[3] at-Tirmidhiy (3004), Ahmad (5674) na al-Bayhaqiy (2948).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 57-59
  • Imechapishwa: 03/10/2018