81 – Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona na Mjuzi. Mikono Yake miwili imekunjuliwa. Allaah alijua kuwa viumbe Wake watamuasi kabla ya kuwaumba. Ujuzi Wake ni kutendeka juu yao. Ujuzi Wake juu yao haikumzuia kuwaongoza katika Uislamu na kuwatunuku kwa sababu ya ukarimu na fadhilah Zake – himdi zote njema zinamstahikia Yeye.

82 – Tambua ya kwamba kuna bishara tatu wakati wa kufa. Kunasemwa:

“Furahi, ee kipenzi cha Allaah kwa radhi na Pepo ya Allaah!”

Kunasemwa pia:

“Furahi, ee adui wa Allaah kwa ghadhabu na Moto wa Allaah!”

Kunasemwa vilevile:

“Furahi, ee mja wa Allaah kwa Pepo baada ya Uislamu!”

Haya yamesemewa na Ibn ´Abbaas.

83 – Tambua kuwa wa kwanza atayemuona Allaah (Ta´ala) Peponi ni kipofu, kisha wanaume halafu wanawake kwa macho ya vichwani mwao, kama alivyosema Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika nyinyi mtamuona Mola Wenu kama mnavyouona mwezi katika usiku wa mwezi mng´aro – hamtosongamana katika kumuona.”[1]

Kuamini haya ni wajibu na kuyapinga ni kufuru.

84 – Tambua ya kwamba haukuwepo uzandiki, ukafiri, shaka, Bid´ah, upotevu wala kutatizika katika dini isipokuwa ni kwa sababu ya elimu ya falsafa na wanafalsafa, mijadala, mizozo na magomvi. Ajabu iliyoje kuona namna ambavyo mtu anathubutu kujishughulisha na mijadala, mizozo na magomvi ilihali Allaah (Ta´ala) anasema:

مَا يُجَادِلُ فِي آيَاتِ اللَّـهِ إِلَّا الَّذِينَ كَفَرُوا

“Habishani katika Aayah za Allaah isipokuwa wale waliokufuru.”[2]

Kwa hivyo ni lazima kwako kujisalimisha, kuridhia juu ya masimulizi na wasimulizi, kukomeka pamoja na kunyamaza.

85 – Inatakiwa kuamini kuwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) atawaadhibu viumbe Motoni kwenye minyororo na pingu na hali Moto uko ndani yao, juu yao na chini yao. Hivo ni kwa sababu Jahmiyyah – akiwemo Hishaam al-Fuutwiy – amedai kwamba Allaah hatoadhibu isipokuwa baada ya kuufikia Moto huo. Huku ni kupingana na Allaah na Mtume Wake.

[1] al-Bukhaariy (554) na (574) na Muslim (633).

[2] 40:04

  • Mhusika: Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin Khalaf al-Barbahaariy (kfk. 329)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh-us-Sunnah, uk. 93-95
  • Imechapishwa: 18/12/2024