Kwa hiyo ikiwa Hadiyth imesimuliwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kutoka vyanzo viwili tofauti, pamoja na kutambua ya kwamba mmoja wao hakuichukua kutoka kwa mwingine, basi inathibitishwa kuwa ni Swahiyh, khaswa ikiwa inatambilika kwamba wapokezi wake si watu wanaojulikana kusema uwongo makusudi na kubwa liliopo ni kwamba makosa yao yanaweza yakawa ya kusahau au ya kukosea kwa bahati mbaya. Kwa mtu anayewafahamu Maswahabah kama Ibn Mas’uud, Ubay bin Ka’b, Ibn ´Umar, Jaabir, Abu Sa’iyd na Abu Hurayrah, basi atatambua kwa uhakika kabisa kwamba hakuna yeyote katika watu hawa ambaye alikuwa anakusudia kumsemea uwongo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), achilia mbali wale Maswahabah waliokuwa na cheo cha juu zaidi. Ni kama ambavyo anamtambua mtu, ambaye anamfahamu ndani na nje kwa muda mrefu, kuwa haibi mali za watu, hapora, hatoi ushahidi wa uongo na kadhalika.
Vivyo hivyo inahusu wanafunzi wa Maswahabah wa Madiynah, Makkah, Shaam na Baswrah. Ambaye anamjua Abu Swaalih ash-Sammaan, al-A‘raj, Sulayman bin Yasaar, Zayd bin Aslam na wengine wa mfano wao, mtu anajua kwa hakika ya kwamba hawakuwa miongoni mwa wale wanaokusudia kubuni uongo katika Hadiyth, achilia mbali wale Maswahabah waliokuwa na cheo cha juu zaidi kama vile Muhammad bin Siyriyn, al-Qaasim bin Muhammad, Sa´iyd bin al-Musayyab, ´Ubaydah as-Salmaniy, ´Alqamah na al-Aswad na wengine wa mfano wao. Kubwa linaloweza kutokea ni makosa ya kibinadamu. Makosa ya kibinadamu na usahaulifu mara nyingi humtokea mtu. Kuna baadhi ya wenye kuhifadhi ambao watu walikuwa wakiwatambua kuwa ni waangalifu sana katika jambo hilo, kama alivyotambulika ash-Sha‘biy, az-Zuhriy, ´Urwah, Qataadah, ath-Thawriy na mfano wao, khaswa az-Zuhriy katika zama zake na ath-Thawriy katika zama zake. Licha ya masimulizi mengi ya Ibn Shihaab az-Zuhriy na kumbukumbu yake pana mtu anaweza kusema kwamba anatambulika kutokukosea.
Kinachokusudiwa hapa ni kwamba Hadiyth ndefu inaposimuliwa kwa mfano kutoka vyanzo viwili tofauti pasi na mwafaka baina ya masimulizi hayo, haiwezekani ikawa ni kosa na uwongo. Kosa kama hilo haliwezi kuwepo katika Hadiyth ndefu na yenye maelezo tofautitofauti, isipokuwa katika hali hiyo linaweza kuwepo katika baadhi ya vipengele. Kwa hiyo mtu mmoja akisimulia Hadiyth ndefu na yenye maelezo tofautitofauti na pia ikasimuliwa tena na mwingine kwa maelezo yaleyale bila makubaliano baina yao, basi haiwezekani kukawa na makosa katika masimulizi yote mawili. Kwa ajili hiyo hapana vyenginevyo makosa huweza kutokea katika baadhi ya vipengele vya kisa, kwa mfano Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliponunua ngamia kutoka kwa Jaabir. Hakika mtu ambaye atazingatia njia mbalimbali za Hadiyth hii basi ataona kwa hakika kuwa ni Swahiyh, japokuwa kuna tofauti za maoni kuhusu bei ya ngamia, kama ambavyo al-Bukhaariy alivyoyabainisha hayo katika ”as-Swahiyh” yake.
- Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 56-59
- Imechapishwa: 01/04/2025
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window) Telegram
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window) WhatsApp
- Click to print (Opens in new window) Print
- Click to email a link to a friend (Opens in new window) Email
- Click to share on Facebook (Opens in new window) Facebook
- Click to share on X (Opens in new window) X
- Click to share on Pocket (Opens in new window) Pocket