Haafidhw ´Abdul-Ghaniy al-Maqdisiy al-Hanbaliy (Rahimahu Allaah) amesema:

189 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kusahau ilihali amefunga ambapo akala au akanywa, basi aikamilishe funga yake. Hakika si vyenginevyo Allaah ndiye kamlisha na kumnywesha.”[1]

MAELEZO

Hadiyth hii ina dalili kuwa aliyesahau amesamehewa. Hivyo akisahau kisha akala au akanywa kisha akakumbuka, basi atakamilisha swawm yake. Swawm yake ni sahihi na hana funga ya kulipa na wala kafara. Lakini ikiwa atakumbuka hali ya kuwa anakula, basi atatema kilicho mdomoni mwake na atakusutua mdomo na atakamilisha swawm yake. Vilevile ikiwa atakumbuka hali ya kuwa anakunywa, basi hatamaliza kunywa, bali atatema maji yaliyomo mdomoni mwake, kisha atajizuia kwa muda uliosalia wa siku. Swawm yake ni sahihi na hana funga ya kulipa wala kafara, kwa sababu usahaulifu hakuna namna ya kuuepuka, bali Allaah ndiye aliyemlisha na kumnywesha.

[1] al-Bukhaariy (1933) na Muslim (1155).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr Dhil-In´am bisharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/444)
  • Imechapishwa: 01/03/2025