Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

122 – Hivyo ni kwa sababu Allaah amedhamini kuwalinda wale wenye kumtambua. Hatowachukulia duniani na Aakhirah kuwa kama wale waliomkanusha, waliokosa mwongozo Wake na hawakupata ulinzi Wake.

MAELEZO

Allaah (Ta´ala) amesema:

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ

“Je, wanadhania wale waliochuma mabaya Tuwafanye wawe sawa na wale walioamini na wakatenda mema na pia sawasawa uhai wao na kufa kwao? – uovu ulioje wanaouhukumu!”[1]

أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ

“Je, Tuwajaalie wale walioamini na wakatenda mema kama wenye kueneza ufisadi ardhini au tuwajaalie wachaji kama waovu?”[2]

Allaah hawalinganishi wale wenye kumtii na wale wenye kumuasi, wala kati ya waumini na makafiri. Bali anamlipa kila mmoja kwa matendo yake. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hatowachukulia duniani na Aakhirah kuwa kama wale waliomkanusha, waliokosa mwongozo Wake na hawakupata ulinzi Wake.”

Bali amepambanua (Subhaanahu wa Ta´ala) kati yao duniani na Aakhirah. Amepambanua kati ya wale wenye kumtii na wale wenye kumuasi, makafiri na waumini – na amefanya hivo duniani na Aakhirah. Amepambanua kati yao duniani inapokuja katika sifa zao, alama zao na matendo yao. Matendo ya mawalii na wale wenye kumtii Allaah sio kama matendo, maneno na mienendo ya maadui wa Allaah. Tazama mienendo yao. Tazama mienendo ya wale wenye kumcha Allaah na waumini na tazama mienendo ya watenda madhambi. Tazama mienendo ya makafiri na wale wakanamungu. Hayo ni hapa duniani.

Huko Aakhirah Allaah atapambanua kati yao kwa njia ya kwamba hawa atawakirimu kwa Pepona wale wengine atawaadhibu kwa Moto. Kwa vile Yeye (Subhaanah) ni Mwingi wa hekima; anakiweka kila kitu mahali pake stahiki. Hatomrehemu isipokuwa tu yule ambaye anastahiki kurehemewa, na wala hatomuadhibu isipokuwa tu yule anayestahiki kuadhibiwa.

Lakini maneno yake mtunzi aliposema:

“Hivyo ni kwa sababu Allaah amedhamini kuwalinda wale wenye kumtambua.”

Hapa kuna mapungufu na kuwatia watu dhana ya kuwa imani ni kule kuwa na utambuzi peke yake, kama wanavosema Murji-ah waliochupa mipaka. Ingelikuwa vyema na wazi zaidi lau angesema:

“Hivyo ni kwa sababu Allaah amedhamini kuwalinda wale wenye kumtii.”

[1]45:21

[2]38:28

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 158-159
  • Imechapishwa: 25/11/2024