120 – Ikiwa hawakutubu, muda wa kuwa watakutana na Allaah hali ya kuwa ni wenye kutambua na wenye kuamini. Atawahukumu vile anavyotaka. Akitaka atawasamehe na kuwasalimisha kutokana na fadhilah Zake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema katika Kitabu Chake:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

Na akitaka kuwaadhibu basi atawaadhibu Motoni kutokana na uadilifu Wake.

MAELEZO

Hii ndio ´Aqiydah ya haki; watenda madhambi makubwa yaliyo chini ya shirki sio makafiri. Wakikutana na Allaah kabla ya kutubia kutokamana na madhambi haya makubwa, basi kuna uwezekano Allaah akaamua kuwaadhibu kwa kiasi cha madhambi yao kisha akawatoa nje ya Moto na kuwaingiza Peponi kutokana na upwekeshaji wao na imani yao –hawatodumishwa Motoni milele. Dalili ya hilo ni maneno Yake Allaah (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”

Hata hivyo maneno yake mtunzi wa kitabu “hali ya kuwa ni wenye kutambua na wenye kuamini” yametajwa kwa njia ya ujumla. Vyema na bora zaidi angesema “hali ya kuwa ni wenye kumwabudu Allaah pekee”.

Ikiwa Allaah atataka basi atawatekelezea matishio pasi na kuwadumisha Motoni milele. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, ´Aqiydah ya haki.

Khawaarij wanadai kuwa watenda madhambi makubwa watadumishwa Motoni milele kwa hali yoyote. Wao wanaona kuwa yule anayeingia Motoni basi hatoki humo.

Murji-ah wanasema kuwa watenda madhambi makubwa hawatogusa Motoni kabisa. Hili ni kosa. Hatuwadhamini kusalimika.

Allaah ndiye atakayeamua cha kuwafanya. Akitaka kuwasamehe basi atawasamehe kwa fadhilah Zake na akitaka kuwaadhibu basi atawaadhibu kwa uadilifu Wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hakuwadhulumu. Amewaadhibu kutokana na matendo yao wenyewe. Allaah hamuadhibu asiyemuasi, mtenda maasi halingani na muumini aliyenyooka:

أَفَنَجْعَلُ الْمُسْلِمِينَ كَالْمُجْرِمِينَ مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ

”Je, Tuwafanye waislamu sawa kama wahalifu? Mna nini nyinyi! Vipi mnahukumu?”[2]

أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ

“Je, Tuwajaalie wale walioamini na wakatenda mema kama wenye kueneza ufisadi ardhini au tuwajaalie wachaji kama waovu?”[3]

Allaah (´Azza wa Jall) amekaripia dhana hiyo na akasema:

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ

“Je, wanadhania wale waliochuma mabaya Tuwafanye wawe sawa na wale walioamini na wakatenda mema na pia sawasawa uhai wao na kufa kwao? – uovu ulioje wanaouhukumu!”[4]

[1]4:48

[2]68:35-36

[3]38:28

[4]45:21

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 156-157
  • Imechapishwa: 24/11/2024