47 – ash-Shaafi´iy (150-204)

196 – Shaykh-ul-Islaam Abul-Hasan al-Hakaariy na Haafidhw Abu Muhammad al-Maqdisiy wamepokea kutoka kwa Abu Thawr na Abu Shu´ayb, kutoka kwa mwenye kunusuru Sunnah Imaam Muhammad bin Idriys ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah), ambaye amesema:

“´Aqiydah ambayo mimi niko juu yake na ambayo nimewaona maswahibah zangu, Ahl-ul-Hadiyth kama vile Sufyaan na Malaik, ni kukiri ya kwamba hapana mungu wa haki mwingine isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah… na kwamba Allaah yuko juu ya ´Arshi Yake juu ya mbingu Zake. Anawakaribia viumbe Vyake Anavyotaka na anashuka kwenye mbingu ya chini Anavyotaka …”

197 – Amepokea kwa cheni ya wapokezi nisiyoitambua kutoka kwa al-Husayn bin Hishaam al-Baladiy ambaye amesimulia kwamba Muhammad bin Idriys ash-Shaafi´iy aliusia yafuatayo:

”Nausia ya kwamba hapana mungu wa haki mwingine isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Mtume wa Allaah… Qur-aan ni maneno ya Allaah (Ta´ala) na kwamba si kiumbe. Allaah (´Azza wa Jall) ataonekana Aakhirah. Waumini watamuona kwa macho yao, waziwazi, na kusikia maneno Yake. Yuko juu ya ´Arshi.”

Cheni ya wapokezi ni dhaifu.

198 – al-Haakim amesema: Nimemsikia al-Aswamm: Nimemsikia ar-Rabiy´ akisema:

”Nimemsikia ash-Shaafi’iy akisimulia Hadiyth kisha bwana mmoja akamwambia: “Je,  unaiamini, ee Abu ´Abdillaah?” Ndipo akajibu: “Ikiwa nitasimulia Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha nisiifanyie kazi, basi nakushuhudisheni ya kwamba akili yangu imepotea.”[1]

199 – Ibn Khuzaymah na wengineo[2] wamesimulia ya kwamba wamemsikia Yuunus akieleza ya kwamba ash-Shaafi´iy amesema:

”Haisemwi juu ya misingi kwa nini? wala vipi?”

200 – Abu Thawr na wengineo wameeleza ya kwamba wamemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

200 – Abu Thawr na wengineo wamesimulia kwamba wamemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

“Hakuna mtu aliyejihusisha na falsafa akafanikiwa.”

201 – ar-Rabiy´ amesimulia kuwa amemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

“Mijadala yenye ubishi katika dini hufanya moyo kuwa mgumu na kuleta chuki.”[3]

202 – Yuunus bin ´Abdil-A´laa amesimulia kuwa amemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

“Allaah (Ta´ala) anayo majina na sifa zilizotajwa ndani ya Kitabu Chake  na ambazo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewasimulia nazo ummah wake. Hakuna yeyote ambaye imemthubutikia hoja anapaswa kuzikanusha.”

Imekuja katika ”al-Mukhtaswar”:

“Allaah (Ta´ala) anayo majina na sifa zilizotajwa ndani ya Kitabu Chake  na ambazo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewasimulia nazo ummah wake. Hakuna yeyote ambaye imemthubutikia hoja anapaswa kuzikanusha. Ikiwa mtu atazikataa baada ya hoja kuthibitika kwake, basi ni kafiri. Ama kabla ya kuthibitika hoja, anapewa udhuru kutokana na ujinga wake, kwa sababu maarifa haya hayawezi kufikiwa kwa akili, tafakuri au fikira. Lazima azithibitishe sifa hizi na kuzikanushia kufanana na viumbe, kama ambavyo Yeye Mwenyewe amejikanushia nazo:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.”[4]

Ameipokea al-Hakaariy na wengineo kwa cheni ya wapokezi yenye wasimulizi wote madhubuti.

Ibn-ul-Qayyim ametaja upokezi huu kwa ukamilifu katika ”Ijtimaa´-ul-Juyuush al-Islaamiyyah”, uk. 59, kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Haatim.

203 – Ibn Abiy Haatim amesema: Nimemsikia ar-Rabiy´ bin Sulaymaan akisema: Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

“Yule mwenye kuapa kwa jina lolote kati ya majina ya Allaah kisha baadaye akavunja kiapo hicho, basi analazimika kutoa kafara, kwa sababu jina la Allaah si kiumbe. Yule mwenye kuapa kwa Ka´bah, Swafaa na Marwah, hakuna juu yake kafara kwa sababu hivi ni viumbe.”

Ni jambo limenukuliwa kwa mapokezi mengi kutoka kwa ash-Shaafi’iy kukemea falsafa na wanafalsafa. Alikuwa ni miongoni mwa watu msitari wa mbele katika kuyafata masimulizi katika katika masuala ya msingi na mataga. Alifariki mwezi wa Rajab mwaka wa 204 huko Misri akiwa na umri wa miaka 54.

[1] Ibn Abiy Haatim katika ”Aadaab-ush-Shaafi´iy”, uk. 93, Abul-Qaasim as-Samarqandiy katika ”al-Amaaliy”, kama ilivyotajwa katika ”al-Muntaqaa” (1/234) ya Abu Hafsw al-Mu’adhdhin, Abu Nu´aym katika ”al-Hilyah” (9/106) na Ibn ´Asaakir (1/10/15) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[2] Miongoni mwao ni Ibn Abiy Haatim katika ”Aadaab-ush-Shaafi´iy”, uk. 233, ambaye ameeleza kuwa baba yake ameongeza kutoka kwa Yuunus, kutoka kwa ash-Shaafi´iy, ambaye amesema:

”Hakika ni kwa tawi tu ndipo mtu huuliza Kwa nini? Ikiwa kipimo chake kwa msingi ni sahihi, basi nayo ni sahihi na hoja imethibitika.'”

[3] Ibn Abiy Haatim katika ”Aadaab-ush-Shaafi´iy”, uk. 185, na Abu Nu´aym katika  ”al-Hilyah” (9/111-112).

[4] 42:11

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Uluww lil-´Aliy al-Ghaffaar, uk. 165-166
  • Imechapishwa: 09/01/2026
  • Taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy