146. Mara kwa kiebrania, mara kwa kiarabu

´Aqiydah ni batili wazi kabisa. Inaonekana kuwa kwa sababu hiyo ndio maana mtunzi wa kitabu hakushughulika kuiraddi. Lakini ni lazima kwetu katika maelezo haya kuelezea baadhi ya Aayah ambazo Ahl-ul-Hadiyth wamezitumia kuthibitisha ubatili wake. Wamesema kwa kifupi ya kwamba kufanya (جعل) haliji kwa maana ya kuumba kila wakati linapotajwa. Mfano wa hayo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَجَعَلْنَا فِي ذُرِّيَّتِهِ النُّبُوَّةَ وَالْكِتَابَ

”Tukamtunukia Ishaaq na Ya’quub na tukafanya katika kizazi chake unabii na Kitabu.”[1]

Hapa kufanya (جعل) hakuna maana ya kuumba kabisa. Uhakika wa mambo ni kwamba Allaah (Ta´ala) ameegemeza neno hili kwa baadhi ya viumbe wake kama vile Yuusuf (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

فَلَمَّا جَهَّزَهُم بِجَهَازِهِمْ جَعَلَ السِّقَايَةَ فِي رَحْلِ أَخِيهِ

”Alipowatayarishia mizigo yao alikitia (جعل) kikopo cha kutekea katika mzigo wa ndugu yake.”[2]

Amesema (Ta´ala) kuhusu washirikina:

وَجَعَلُوا الْمَلَائِكَةَ الَّذِينَ هُمْ عِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ إِنَاثًا

“Wakawafanya (وَجَعَلُوا) Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa huruma, kuwa ni wa kike!”[3]

Je, ina maana kwamba washirikina ndio wameumba Malaika? Allaah ametakasika kutokana na tafsiri za wazushi kutakasika kukubwa! Kwa hivyo yakishabainika haya ni lazima kueleza maana ya neno hilo kwa kuzingatia muktadha lililotajwa. Hebu chukua kwa mfano maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّا جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لَّعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ

”Hakika Sisi Tumekifanya (جَعَلْنَاهُ) kisomeke kwa Kiarabu ili mpate kutia akilini.”

Hapana shaka kwamba Aayah inazungumzia Qur-aan. Qur-aan ni maneno yake Allaah (Ta´ala) pasi na shaka. Maneno Yake ni sifa miongoni mwa sifa Zake. Sifa Zake zote ni za milele, hazikuumbwa, kama ilivyo dhati Yake Mwenyewe na kwa ajili hiyo haitofaa kufasiri neno hili kwa maana inayopingana na mambo haya yenye uhakika. Kwa vile Allaah (Ta´ala) anazijua lugha zote na anaweza kusema Anavyotaka, wakati Anaoutaka – Anazungumza kiarabu pale Anapotaka na kiebrania pale Anapotaka – hivyo basi maana ya Aayah isemayo:

إِنَّا جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لَّعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ

”Hakika Sisi Tumekifanya (جَعَلْنَاهُ) kisomeke kwa Kiarabu ili mpate kutia akilini.”

ametamka Qur-aan kwa kiarabu kama ambavo ametamka Tawraat kwa kiebrania. Kwa sababu Amemtuma kila Mtume kwa lugha ya watu wake ili apate kuwabainishia. kama alivyosema Allaah (Ta´ala) ndani ya Kitabu Chake. Hivyo basi maana ya Aayah hiyo ni kuitoa katika lugha moja kwenda katika lugha nyingine, si kwamba ameiumba. Tazama kitabu chake ”ar-Radd ´alaal-Mariysiy”, uk. 123-124.

[1] 29:27

[2] 12:70

[3] 43:19

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Uluww lil-´Aliy al-Ghaffaar, uk. 175
  • Imechapishwa: 09/01/2026
  • Taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy