Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

116 – Imani ni kule kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na makadirio, ya kheri na shari yake, tamu yake na chungu yake, inatoka kwa Allaah (Ta´ala).

117 – Sisi tunayaamini yote hayo.

MAELEZO

Imani maana yake ni kutamka kwa ulimi, kusadikisha kwa moyo na matendo ya viungo vya mwili. Inazidi kwa utiifu na inapungua kwa kuasi. Yale yaliyotajwa na mtunzi (Rahimahu Allaah) hapa ni nguzo za imani. Wakati Jibriyl (´alayhis-Salaam) alipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu imani akajibu:

”Kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na kuamini Qadar, kheri na shari yake.”[1]

Imani inangazi nyingi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani ni tanzu sabini na kitu. Ya juu yake kabisa ni neno “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” na ya chini yake ni kuondosha chenye kuudhi njiani. Hayaa ni tanzu pia ya imani.”[2]

Hata hivyo mambo haya sita ni nguzo na misingi ambayo dini inasimama juu yake. Tumeshatangulia kutaja kuhusu kumuamini Allaah, Malaika Wake, Mitume Yake, Vitabu Vyake na siku ya mwisho.

Ni lazima kuyaamini yote haya. Yule anayepinga kitu katika nguzo hizi sio muumini, kwa sababu kutakuwa kumekosekana nguzo miongoni mwa nguzo za imani.

[1] Muslim (8).

[2]al-Bukhaariy (9) na Muslim (35).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 152-153
  • Imechapishwa: 20/11/2024