Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

115 –Waumini wote ni mawalii wa Mwingi wa huruma. Wabora wao mbele ya Allaah ni wale watiifu na wanaoifuata Qur-aan zaidi.

MAELEZO

Ni haki. Waumini wote ni mawalii wa Allaah. Kwa msemo mwingine ni wapenzi wa Allaah. Allaah anawapenda waumini, anawapenda wenye kumcha, anawapenda wafanyao matendo mema, anawapenda wenye kutubu na anawapenda wanaojitwahirisha. Vilevile anawachukia makafiri na watenda madhambi. Allaah anapenda na anachukia kutokana na matendo ya watu.

Kila muumini anakuwa ni walii wa Allaah. Uwalii huu unatofautiana. Baadhi yao ni wabora kuliko wengine. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa wanamcha.”[1]

Miongoni mwa watu wako ambao ni mawalii wa Allaah kikamilifu, wengine kwa upungufu. Wengine ni maadui wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na wako mbali Naye. Kila ambaye ana imani na kumcha Allaah basi ni walii wa Allaah, lakini uwalii huu unatofautiana kutegemea na matendo. Wako ambao ni mawalii kikamilifu. Wengine ni mawalii wa Allaah kwa upande mmoja ambao ni wale waumini watenda madhambi; ni walii kwa Allaah kutokana na utiifu wake na ni adui wa Allaah kutokana na maasi na uhalifu wake. Wako wengine ambao ni maadui wa Allaah kikamilifu, nao ni wale makafiri na washirikina.

Hii ndio haki. Hata hivyo wako wanaosema kuwa Allaah hana mawalii isipokuwa tu wale waliojengewa juu ya makaburi yao mabanda au makuba na wale ambao hawakujengewa mabanda na makuba sio mawalii. Namna hiyo ndivyo wanavyofikiri waabudia makaburi – fikira yao ni batili.

[1]10:62-63

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 151-152
  • Imechapishwa: 20/11/2024