14. Ulazima wa kuweka nia usiku katika swawm ya faradhi

Tambueni ya kwamba nia katika kufunga ni jambo la lazima na ni sharti la kusihi kwake, kama ilivyo sharti kwa kusihi kwa ´ibaadah zote. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika si vyengineyo matendo yanategemea nia na kila mmoja atalipwa kutokana na vie alivyonuia.”[1]

Nia hiyo ni kwamba mtu aitakidi mwanzoni mwa swawm kwamba anafunga Ramadhaan, anafunga deni, anafunga nadhiri au kafara.

Wakati wa nia ya swawm ya wajibu kwa aina zake zote ni usiku, ni mamoja iwe mwanzo wa usiku, katikati yake au mwisho wake. ad-Daaraqutwniy kwa cheni yake ya wapokezi kupitia kwa ´Amrah kutoka kwa ´Aaishah kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Yeyote asiyelaza [nia ya] swawm kabla ya kuchomoza kwa alfajiri basi hana swawm.”[2]

Ibn ´Umar amepokea kupitia kwa Hafswah ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote asiyelaza [nia ya] swawm kabla ya alfajiri, basi hana swawm.”

Imekuja katika tamko jengine:

“Yeyote asiyekusudia… ”

Kwa maana asiyefanya azma.

“… kufunga tangu usiku, basi hana swawm.”[3]

Kwa kuwa mchana wote unawajibika kufungwa. Ikipita sehemu ya mchana bila kuwepo nia basi swawm ya siku nzima haisihi, kwa sababu nia hairejei nyuma kwa yaliyopita.

[1] Muslim (1907).

[2] ad-Daaraqutwniy (02/172) na al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (04/202) ambaye amesema:

”Cheni yake ya wapokezi wote ni wenye kuaminika.”

[3] Ahmad (06/287), Abu Daawuud (2454) na at-Tirmidhiy (730).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 22
  • Imechapishwa: 02/02/2026