Lengo la kumi na nne: Kuhakikisha ukatikati

Miongoni mwa malengo ya hajj ni kuhakikisha ukati na kati ambao ndio pambo la dini hii na uzuri wa Shari´ah. Dini ya Allaah (´Azza wa Jall) ni dini ya kati na kati isiyokuwa ndani yake na kuchupa mipaka wala kuzembea. Allaah (Ta´ala) amesema:

كَذَٰلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا

“Ndivyo hivyo Tumekufanyeni ummah kati na kati na adilifu.”[1]

Bi maana mashahidi na waadilifu. Hakuna kupetuka mipaka wala uzembeaji. Uzuri wa mambo ni yale ya kati na kati yasiyokuwa na kuchupa mipaka wala kuzembea. Makusudio ya maneno Yake (Subhaanah):

أُمَّةً وَسَطًا

“… ummah kati na kati na adilifu.”

bi maana mashahidi na waadilifu. Hawamili kutoka katika haki; si kwenda katika kuvuka mipaka wala kwenda katika uzembeaji. Bali wanakuwa kati na kati. Hajj imejaa visimamo vitukufu na mazingatio matukufu ambayo yanamwelekeza mtu katika umuhimu wa kuwa mkati na kati na visimamo ambavyo vinafahamisha umuhimu wa ukati na kati. Miongononi mwa visimamo hivi katika mlango huu mkubwa ni kutazama uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mwenendo wake katika kurusha vijiwe kwa mujibu wa yale yaliyothibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya hapo mtu atazame hali za watu pamoja na kulinganisha mwenendo wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika hali zao hazitoki kati ya kuchupa mipaka na kuzembea – isipokuwa tu wale waliowafikishwa na Allaah, akawakirimu katika kulazimiana na Sunnah zake, kufuata mwongozo wake na nyayo zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

al-Bayhaqiy amepokea katika “as-Sunan” yake kupitia kwa Ibn ´Abbaas ambaye amesimulia:

“al-Fadhwl bin ´Abbaas amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinambia katika asubuhi ya siku ya Nahr: “Hebu niokotee vijiwe ambapo nikamukotea vijiwe kiasi cha vijiwe vinavyotumika katika Khadhf.” Akasema: “[Mrushe] kwa mfano wa vijiwe hivi, [mrushe] kwa mfano wa vijiwe hivi. Tahadharini na kuchupa mipaka. Kwani hakika hakuna kilichowaangamiza wale waliokuwa kabla yenu isipokuwa ni kuchupa mipaka katika dini.”

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kwa mfano wa vijiwe hivi” bi maana vijiwe ulivyookotewa ambavyo vimewekwa kipimo chake na Hadiyth hii. Tamko hili halikusudii kijiwe kidogo ambacho hakiingii katika Khadhf. Wala hakingii vilevile katika kiwango kikubwa ambacho ni jiwe. Kilichowekwa katika Shari´ah ni kuwa kati na kati. Pamoja na kuwa jambo hili ameliweka wazi na kulibainisha sana, basi hakika ukiyalinganisha hayo na hali za baadhi ya waislamu ambao hawazijui Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) utaona kutoka kwao mambo ya ajabu katika mlango huu baina ya kuchupa mipaka na kuzembea, kuongeza na kupunguza. Haki iko kati na kati. Muislamu hatakiwi kupunguza katika Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama wanavofanya wenye kuzembea, na wala haongezi juu yake, kama wanavofanya wenye kuchupa mipaka na kupindukia. Bali anatakiwa mwadilifu na mkati na kati.

Maneno yake: “Tahadharini na kuchupa mipaka” ni yenye kuenea na yamekusanya aina zote za kuchupa mipaka katika I´tiqaad na matendo. Kwa sababu kinachozingatiwa ni kule kuenea kwa matamshi na si sababu ya matukio. Muislamu amekatazwa kuchupa mipaka katika hali zake zote na ameamrishwa kufuata nyayo za Mtume mkarimu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kufuata Sunnah zake katika hali zake zote.

Sura hii inayotudhihirikia katika mahali hapa kwa mfano kama huu ulio wazi unatuwekea wazi ukati na kati wa dini katika mambo yote ya dini. Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) iko kati na kati baina ya kuchupa mipaka na kuzembea. Hivyo muislamu anatoka katika hajj yake akiwa na faida kubwa na lengo tukufu alilolichuma katika hajj kwa njia ya kwamba matendo yake siku zote yanakuwa kati kwa kati; hayana kuchupa mipaka wala kuzembea.

Ukati na kati unakuwa kwa kule kwenda sambamba na Sunnah. Kwa hivyo atahadhari kwelikweli yule mwenye kuivuka Sunnah. Ni mamoja iwe kwa kuchupa mipaka au kwa kuzembea. Shaytwaan ni mwenye kupupia sana kumwondosha mja wa Allaah muumini kutoka katika msitari na kumuweka mbali na njia ya Allaah iliyonyooka. Matokeo yake ima anamtupa katika kuchupa mipaka au katika uzembeaji. Shaytwaan hajali ni kipi kati ya hayo mawili atamtupa ndani yake. Baadhi ya Salaf wamesema:

“Allaah hakuamrisha amri yoyote isipokuwa shaytwaan anakuwa na njia mbili; ima katika kuzembea na kupunguza au katika kuzidisha na kuvuka mipaka. Hajali ni lipi katika hayo atayompata.”

Shaytwaan amemkalia muislamu katika njia zake zote. Hachoki na wala hakati tamaa ya kumfanyia vitimbi na kumpoteza kwa kiasi cha uwezo wake kumuondoa kutoka katika njia iliyonyooka na uongofu wa wazi.

Kuwa kati na kati katika mambo yote na kujiweka mbali na kupetuka mipaka na kuzembea ndio mfumo barabara na njia iliyonyooka ambayo inatakiwa kufuatwa na waumini wote. Allaah ndivo alivyoamrisha katika Kitabu Chake. Mtume pia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndivo alivyoamrisha. Ukati na kati wa kweli ni mtu kufuata kile kiwango kilichowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kuwawekea waja Wake kwa njia ya kwamba kusiingizwe kile kisichokuwa ndani yake na wala kisitolewe kile kinachotakiwa kuwa ndani yake. Kwa haya Allaah amewasifu waumini. Dini ya Allaah iko kati na kati baina ya yule mwenye kupetuka mipaka na mwenye kuzembea. Watu bora ni wale ambao wamejiondoa kutoka katika upungufu wa wale wazembeaji na wala hawakufuata nyayo za wale waliovuka mipaka. Kinyume chake wamefuata uongofu wa bwana wa Mitume, mbora wa Mola wa walimwengu na kiigizo cha watu wote; Muhammad bin ´Abdillaah – swalah na salaam zimwendee yeye, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

[1] 02:143

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 69-75
  • Imechapishwa: 22/08/2018