14. Imani ya kuamini Qadhwaa´ na Qadar ina daraja ngapi na ni zipi?

´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 14: Imani ya kuamini Qadhwaa´ na Qadar ina daraja ngapi na ni zipi?

Jibu: Ni nne. Imani ya mtu haitimii mpaka aziamini zote:

1 – Kuamini kuwa Allaah juu ya kila kitu ni mjuzi na ujuzi Wake umekizunguka kila kitu.

2 – Kuamini kuwa ameyaandika yote hayo katika Ubao uliohifadhiwa.

3 – Kuamini kuwa kila kinachopitika, basi kinapitika kwa matakwa na uwezo Wake. Anachotaka, huwa, na asichotaka, hakiwi.

4 – Kuamini kuwa Allaah amewaacha waja watende kwa utashi wao. Wanatenda kwa khiyari yao wenyewe, kwa kutaka kwao na kwa nguvu zao. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Je, hujui kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yameandikwa katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”[1]

لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke. Na hamtotaka isipokuwa Atake Allaah, Mola wa walimwengu.”[2]

MAELEZO

Imani ya kuamini Qadhwaa´ na Qadar ina daraja nne:

1 – Kuamini elimu ya Allaah yenye kuenea na kwamba elimu Yake imekienea kila kitu. Allaah (´Azza wa Jall) ameyajua yote hayo kwa upambanuzi. Anajua ni lini na wapi mambo yatatokea. Amemjua kila mmoja katika sisi na viumbe wengine wote hadi siku ya Qiyaamah; mwaka wake wa kuzaliwa na maeneo yake ya kuzaliwa.

Ameyajua mambo watakayoyafanya, ni lini watayafanya na ni wapi watayafanya. Amejua ni wapi, lini na ni vipi kila mmoja katika sisi atakufa na kama atakufa kwa kuuliwa, maradhi, kifo cha kawaida, kuchomeka kwa moto, kuzama ndani ya maji, kuangukiwa na jengo na mfano wa hayo. Yote hayo ameyajua Allaah. Allaah amekijua kila kitachotokea katika ulimwengu. Ameyajua kabla hayajatokea, ameyakadiria na ameyaandika. Kuna dalili nyingi zisizodhibitika juu ya hayo. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa upo katika Kitabu, kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”[3]

2 – Kuamini kwamba ameyaandika yote hayo katika Ubao uliohifadhiwa. Amesema (´Azza wa Jall):

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

”Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa Qadar.”[4]

Imekuja katika Hadiyth:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika.” Ikasema: “Niandike nini?” Akasema: “Andika kila kitachokuwa mpaka kisimame Qiyaamah.”[5]

Kwa hiyo kalamu imeandika makadirio kwa amri ya Allaah (´Azza wa Jall).

3 – Kila chenye kutokea ni kwa matakwa na uwezo Wake. Anachotaka, huwa, na asichotaka, hakiwi. Hakutokei kitu katika ulimwengu huu pasi na utashi wa Allaah. Vinginevyo ingekuwa na maana kuwa amri Yake ni yenye kushindwa. Ilihali Allaah ni mwenye kushinda na sio mwenye kushindwa. Allaah ndiye Mwenye kudhibiti kila kitu na sio mwenye kudhibitiwa. Yeye ndiye kawaumba viumbe na akaumba matendo yao. Ameeleza (Ta´ala) kuwa Ibraahiym (´alayhis-Salaam) alisema kuwaambia watu wake:

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah amekuumbeni pamoja na vile mnavovifanya.”[6]

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

”Hamtotaka isipokuwa atake Allaah, Mola wa walimwengu.”[7]

وَنَفْسٍ وَمَا سَوَّاهَا فَأَلْهَمَهَا فُجُورَهَا وَتَقْوَاهَا

”Naapa kwa nafsi na Aliyeitengeneza, kisha akaitambulisha uovu wake na uchaji wake.”[8]

4 – Ameyafanya makadirio yao kufanya kazi kwa njia ya kuwaacha waja wayafanye. Ametaka wayafanye yale Aliyowakadiria. Hayo ndio yale ambayo huitwa makadirio ya siku. Kwa sababu kuna makadirio yafuatayo:

1 – Makadirio yenye kuenea yaliyoandikwa katika Ubao uliohifadhiwa. Huko Allaah ndiko kaandika makadirio yote.

2 – Makadirio ya umri yanayoandikwa wakati kinapoumbwa kipomoko. Makadirio haya yamechukuliwa kutoka katika yale makadirio yenye kuenea.

3 – Makadirio ya mwaka yanayoandikwa katika usiku wa Makadirio katika kila mwaka.

4 – Makadirio ya kila siku ambayo ni matekelezo ya hayo makadirio yote yaliyotangulia. Kwa mfano leo Allaah amekadirio utakula chakula fulani, utaenda mahali fulani na mengineyo mpaka kufa kwako, pasi na kujali namna ya kifo chako. Imekuja katika Hadiyth:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika.” Ikasema: “Niandike nini?” Akasema: “Andika kila kitachokuwa mpaka kisimame Qiyaamah.”

Imepokelewa pia kwamba Malaika huyaandika matendo ya waja:

“Wanapopanda juu mbinguni basi wanayadhihirisha katika Ubao uliohifadhiwa na wanayakuta ni yenye kwenda sambamba nayo na hayatofautiani hata kidogo.”

[1] 22:70

[2] 81:28-29

[3] 57:22

[4] 54:49

[5][5] Abu Daawuud (4700) na at-Tirmidhiy (2155). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (2017).

[6] 37:96

[7] 81:29

[8] 91:7-8

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 80-83
  • Imechapishwa: 18/10/2021