14. Cheni ya wapokezi inayokosa Swahabah (المرسل)

Hadiyth ambazo anakosekana Swahabah katika cheni ya wapokezi (المرسل) na zikapokelewa kwa njia nyingi, kwa namna ya kwamba zisingeweza kusimuliwa kwa njia hiyo kwa makusudi na kwa bahati, basi huwa ni Swahiyh kwa yakini. Hii ni kwa sababu nukuu iliyosimuliwa inaweza kuwa ni ya kweli inayoenda sambamba na tukio au ya uwongo iliyobuniwa na mpokezi ima kwa makusudi au kwa kukosea. Ikiwa imesalimika kutokana na uwongo wa makusudi na makosa, basi bila shaka ni ya kweli.

Ikiwa Hadiyth imesimuliwa kutoka kwa pande mbili au zaidi na inafahamika kuwa wasimuliaji hawakupanga kubuni khabari hiyo na pia ikatambulika ya kwamba mambo kama hayo haiwezekani kwa kawaida kukubaliana kwa kupanga, basi inakuwa wazi kuwa ni ya sahihi. Mfano mtu mmoja anasimulia tukio lililotokea na akaeleza kwa undani maneno na matendo yaliyotokea, kisha akaja mtu mwingine ambaye inatambulika ya kwamba hakupanga naye ambapo akasimulia vivyo hivyo kwa undani uleule. Hii inaleta yakini kuwa tukio hilo ni la kweli kwa ujumla. Kwani ingelikuwa wote wawili wamesema uwongo kwa makusudi au kimakosa, basi tukio hilo kwa kawaida lisingesimuliwa sawasawa kwa undani na wote wawili. Kawaida haiwezekani kwa watu wawili kuelezea kitu kama hicho bila kukubaliana hapo awali. Ni kweli kwamba mtu anaweza kutunga mstari mmoja na mtu mwingine akaweza kutunga msitari kama huo, au mtu anaweza kubuni uwongo fulani na mwingine naye akaja na uwongo wa aina hiyo. Lakini ikiwa mtu huyo atatunga shari refu lenye vipengele mbalimbali, lenye kibwagizo vina maalum na urefu wa kupindukia, basi si kawaida kwamba atakuja mtu mwingine kulitunga kwa namna sawa kabisa kwa maneno na maana bila kuiiga kutoka kwa wa kwanza. Hali hii hufanya iwe wazi kwamba ameichukua kutoka kwa yule wa kwanza. Mtu anaweza kutunga shairi moja au la mstari mmoja, na mtu mwingine akaweza kutunga shairi lingine linalofanana. Au mtu anaweza kubuni uongo fulani, na mwingine naye akaja na uongo wa aina hiyo. Lakini, ikiwa mtu atatunga kasida ndefu yenye vipengele mbalimbali, mizani sahihi, vina maalum, na urefu wa kupindukia, basi si kawaida mtu mwingine kuitunga kwa namna sawa kabisa kwa maneno na maana bila kuiiga kutoka kwa wa kwanza. Hali hii hufanya iwe wazi kwamba ameichukua kutoka kwa wa kwanza. Kadhalika ikiwa mtu atasimulia Hadiyth ndefu yenye vipengele na maelezo mengi na akaja mwingine akaisimulia kwa namna ileile; ima wamekubaliana  juu yake, mmoja wao ameichukua kutoka kwa mwingine au Hadiyth hiyo ikawa ni ya kweli. Kwa njia hii mtu anaweza kutambua usahihi wa masimulizi mengi ambayo yanatoka katika vyanzo tofauti na yenye kufanana kwa undani, hata kama chanzo kimoja hakitoshi kuthibitishwa ima kwa sababu kuna Swahabah anayekosekana katika cheni ya wapokezi au udhaifu wa mpokezi. Hata hivyo njia hii haiwezi kutumika kuthibitisha matamshi mahsusi au maelezo ya kina ambayo yatambuliki kwa njia hii. Zinahitaji njia nyingine inayozithibitisha kama vile yale matamshi mahsusi na maelezo ya kina. Kwa ajili hiyo imethibiti kwamba vita vya Badr vilitokea kabla ya Uhud, na kwamba ilikuwa kabla ya Uhud, kwa njia za mapokezi mengi. Bali ni jambo linalotambulika pasi na shaka kwamba Hamzah, ´Aliy, na ´Ubaydah walipambana na ´Utbah, Shaybah na al-Waliyd, na kwamba ´Aliy alimuua al-Waliyd, kwamba Hamzah alimuua mpinzani wake, ingawa kuna shaka ikiwa mpinzani wake alikuwa ´Utbah au Shaybah.

Msingi huu unapaswa kutambulika, kwani una manufaa sana katika kuthibitisha masimulizi mengi ya Hadiyth, tafsiri ya Qur-aan, historia ya vita, maneno na matendo ya watu na mengineyo.

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 54-56
  • Imechapishwa: 01/04/2025