13. Vipi mtu anatakiwa kuwaamini Mitume kwa njia ya upambanuzi?

´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 13: Vipi mtu anatakiwa kuwaamini Mitume kwa njia ya upambanuzi?

Jibu: Ni juu yetu kuwaamini Manabii na Mitume wote ambao unabii na ujumbe wao umethibiti. Imani hii inatakiwa iwe kwa njia ya ujumla na upambanuzi.

Tunaamini kuwa Allaah amewateua kwa Wahy na kuwatumwa Kwake.

Amewafanya kuwa ni wakati kati baina Yake na viumbe Wake katika kufikisha dini na Shari´ah Yake.

Amewapa nguvu kwa alama zenye kuthibitisha kuwa ni wakweli na usahihi wa yale waliyokuja nayo.

Wao ndio viumbe wakamilifu kabisa inapokuja katika elimu, matendo, ukweli, wema na tabia.

Allaah amewakhusisha kwa fadhila walizopwekeka nazo na amewatakasa na kila sifa mbaya.

Wamekingwa na kukosea katika yale yote wanayofikisha kutoka kwa Allaah.

Hakuna kinachochukua nafasi katika maelezo na ufikishaji wao isipokuwa haki na ya usawa.

Ni wajibu kuwaamini wote na yale yote waliyopewa kutoka kwa Allaah. Vilevile ni wajibu kuwapenda, kuwaheshimu na kuwaadhimisha.

Tunaamini kuwa mambo yote haya ni wajibu kumtekelezea nayo Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia kamilifu zaidi.

Ni wajibu kumjua na kujua yale aliyokuja nayo katika Shari´ah kwa njia ya jumla na ya upambanuzi, kadri vile mtu atakavyoweza. Vilevile ni wajibu kuamini hilo, kushikamana nalo na kumtii katika kila kitu alichokielezea, kukiamrisha na kukikataza.

Yeye ndiye Nabii wa mwisho. Hakuna Nabii mwengine baada yake. Shari´ah yake imezifuta Shari´ah zingine zote na itaendelea kufanya kazi mpaka siku ya Qiyaamah.

Imani ya kumuamini haitimii mpaka mja atambue kuwa yote aliyokuja nayo ni haki.

Haiwezekani dalili ya kiakili, kihisia au nyengine ikapingana na yale aliyokuja nayo. Uhakika wa mambo ni kuwa akili timamu na mambo ya kihisia ya kihakika vyote viwili vinathibitisha kuwa Mtume ni mkweli na anazungumza haki.

MAELEZO

Hii ina maana kwamba ni lazima kuamini Manabii na Mitume yote waliyotajwa kwa majina na Allaah (´Azza wa Jall). Ni lazima kuwaamini na kuamini majina yao na kuzitambua nafasi zao. Mfano wao ni wale Mitume bora watano: Nuuh, Ibraahiym, Muusa, ´Iysaa na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tunaamini kuwa hawa ndio Mitume bora na kwamba wabora zaidi katika wao ni Ibraahiym na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam).

Tunaamini pia Mitume wengine waliotajwa kama mfano wa Huud, Swaalih, Shu´ayb, Luutw, Ayyuub, Yahyaa, Zakariyyaa, Ismaa´iyl, Ishaaq na Ya´quub. Wote hawa ni Mitme waliofikisha ujumbe kutoka kwa Allaah. Pia tunawaamini wale ambao hawakutajwa kwa njia ya ujumla. Ahmad amepokea kupitia kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Ee Mtume wa Allaah! Manabii ni wangapi?” Akajibu: “124.000 ambapo miongoni mwako kuna Mitume 315. Ni idadi kubwa.”[1]

Katika tamko la Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake imekuja:

“Ee Mtume wa Allaah! Mitume walikuwa wangapi?” Akajibu: “120.000.” Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mitume walikuwa wangapi katika hao?” Akajibu: “313. Ni idadi kubwa.”[2]

Sisi tunaamini kuwa wapo Mitume ambao visa vyao havikuelezwa na Mitume wengine ambao visa vyao vimeelezwa. Tunawaamini wote hawa. Wale ambao wametajwa kwa majina tunawaamini kwa majina yao na wale ambao hawakutajwa kwa majina yao tunawaamini kwa ujumla. Allaah alisema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ مِنْهُم مَّن قَصَصْنَا عَلَيْكَ وَمِنْهُم مَّن لَّمْ نَقْصُصْ عَلَيْكَ

“Hakika Tumewapeleka Mitume kabla yako; miongoni mwao wako Tuliokusimulia na miongoni mwao wako ambao hatukukusimulia.”[3]

Tunaamini kuwa Allaah amewafanya kuwa maalum kwa mwongozo na ujumbe Wake:

اللَّـهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ

“Allaah anajua zaidi wapi aweke ujumbe Wake.”[4]

وَمَا أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ إِلَّا رِجَالًا نُّوحِي إِلَيْهِمْ ۖ فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

”Hatukutuma kabla yako isipokuwa wanaume Tunaowafunulia Wahy, basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa hamjui.”[5]

Tunaamini kuwa Allaah amewafanya kuwa waunganishi baina Yake na baina ya viumbe Wake katika kuifikisha dini na Shari´ah Yake. Amewatia nguvu kwa alama zinazofahamisha juu ya ukweli kwao na ukweli wa yale waliyokuja nayo. Aliufanya moto kuwa baridi na yenye salama kwa Ibraahiym. Allaah alimfanya Muusa kuwa na bakora na mkono. Akamfanya Swaalih kuwa na ngamia. ´Iysaa alikuwa ni mwenye kuwapa uhai wafu kwa idhini ya Allaah na akiunda kwa udongo kitu kwa sura ya ndege na kinakuwa ndege kwa idhini ya Allaah.

Wapo Mitume wengine ambao hawatuwajui. Hata hivyo ni lazima kuamini kuwa kila Mtume Allaah alimpa miujiza inayofahamisha ukweli wa ujumbe wake. Mitume ndio viumbe wenye elimu kamilifu zaidi na matendo. Wao ndio watu wakweli zaidi. Wao ndio viumbe wenye nyoyo zenye uchaji zaidi na wenye tabia kamilifu zaidi. Allaah amewafanya kuwa maalum kwa fadhilah mbalimbali ambazo hakuna yeyote anaweza kulingana nao. Amewatakasa kutokamana na kila sifa mbaya. Wamekingwa na kukosea katika kila wanachokifikisha kutoka kwa Allaah.

Mitume kukukingwa na kukosea kunaanza tangu wakingapi wadogo au kukingwa na kukosea kunaanza baada ya kutumilizwa? Hapana shaka kwamba wamekingwa na kukosea katika yale wanayoyafikisha kutoka kwa Allaah.

Tunaamini kuwa yale wanayoyasema na kuyafikisha si vyenginevyo isipokuwa ni haki. Allaah (´Azza wa Jall) amemweleza Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kumwambia:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ وَلَا نَبِيٍّ إِلَّا إِذَا تَمَنَّىٰ أَلْقَى الشَّيْطَانُ فِي أُمْنِيَّتِهِ فَيَنسَخُ اللَّـهُ مَا يُلْقِي الشَّيْطَانُ ثُمَّ يُحْكِمُ اللَّـهُ آيَاتِهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ لِّيَجْعَلَ مَا يُلْقِي الشَّيْطَانُ فِتْنَةً لِّلَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ وَالْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُمْ ۗ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَفِي شِقَاقٍ بَعِيدٍ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote na wala Nabii yeyote isipokuwa [anaposoma Kitabu cha Allaah au kufikisha ujumbe] shaytwaan hujaribu kufanya nia yake iwe ya mashaka, lakini Allaah hufuta yale anayoyatupia shaytwaan kisha Allaah anathibitisha Aayah Zake – na Allaah ni Mjuzi wa kila kitu, Mwenye hekima wa yote. Ili Afanye yale aliyoyatupa shaytwaan kuwa ni fitina kwa wale wenye maradhi kwenye nyoyo zao na nyoyo zao ni susuwavu. Na hakika madhalimu bila shaka wamo katika upinzani wa mbali.”[6]

Pindi shaytwaan anapojaribu kuchafua kitu katika usikizi wa Mitume basi Allaah (´Azza wa Jall) anakifuta, anakitoa nje na kuthibitisha ukweli.

Ni lazima kuwaamini Mitume wote na yale yote waliyokuja nayo kutoka kwa Allaah, kuwapenda, kuwaheshimu na kuwatukuza. Tunaamini kuwa mambo haya ni wajibu kwetu na khaswa inapokuja kwa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mambo yakishakuwa hivo kwamba ni lazima kwetu kuwapenda Mitume wote, basi ni lazima vilevile kumpenda yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zaidi kuliko mwengine yeyote. ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Hakika wewe unapendwa zaidi kwangu kuliko kila kitu isipokuwa tu nafsi yangu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake, mpaka uwe ni mwenye kunipenda zaidi kuliko nafsi yako.” Ndipo ´Umar akasema (Radhiya Allaahu ´anh): “Hivi sasa nakupenda zaidi kuliko nafsi yangu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hivi sasa, ee ´Umar.”[7]

Vilevile ni lazima kuwa na utambuzi juu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na utambuzi juu ya ujumbe wake kiasi mtu atakavyoweza, kuuamini, kulazimiana nao na kumtii (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kila jambo, hali ya mtu kusadikisha khabari zake, kutekeleza amri zake na kujiepusha na makatazo yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Hatukutuma Mtume yeyote isipokuwa atiiwe kwa idhini ya Allaah.”[8]

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika amekujieni Mtume anayetokana na nyinyi wenyewe, ni magumu juu yake yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni, mwenye huruma mno na mapenzi tele kwa waumini.”[9]

فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Basi wale waliomuamini na wakamtukuza na wakamnusuru na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye, hao ndio wenye kufaulu.”[10]

Pia tunaamini kuwa yeye ndiye Mtume wa mwisho na kwamba hakuna Mtume mwingine baada yake. Shari´ah yake imeifuta kila Shari´ah na ni yenye kuendelea kufanya kazi mpaka siku ya Qiyaamah. Imani ya kumwamini haitimii mpaka mja atambue kuwa kila alichokuja nacho na kukifisha ni haki. Amesema (Ta´ala):

ثُمَّ جَعَلْنَاكَ عَلَىٰ شَرِيعَةٍ مِّنَ الْأَمْرِ فَاتَّبِعْهَا وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ إِنَّهُمْ لَن يُغْنُوا عَنكَ مِنَ اللَّـهِ شَيْئًا ۚ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۖ وَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُتَّقِينَ

“Kisha Tukakuwekea Shari´ah ya mambo; hivyo basi ifuate na wala usifuate matamanio ya wale wasiotambua. Hakika wao hawatokufaa chochote mbele ya Allaah na hakika madhalimu ni walinzi wanaoshirkiana wao kwa wao, na Allaah ni Mlinzi wa wale wenye kumcha.”[11]

Ni muhali kwamba dalili ya kiakili, ya kihisia au nyengineyo igongane na yale yaliyokuja katika Shari´ah ambayo ndio njia ilionyooka. Mambo ya kihisia yanamshuhudilia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa ni mkweli na wa haki. Bali katika Shari´ah yenyewe zipo khabari zinazofahamisha juu ya ukweli wake na haki ya ujumbe wake. Miongoni mwa hayo ni pale ilipoeleza juu ya kufunguliwa mji wa Makkah, Khawaarij  wanaisoma Qur-aan pasi na kuvuka koo zao na moto unaotokea maeneo ya Hijaaz na kuangaza hadi Shaam. Moto huo ulijitokeza maeneo ya njenje ya Madiynah mwaka wa 656. Kadhalika imeeleza kuwa Ummah wake utafuata nyayo za wale waliokuwa kabla yao na kuhusu kukaribiana kwa zama kwa mwendo mfupi uliotokea katika zama zetu hizi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakitosimama Qiyaamah mpaka zikaribiane zama. Mwaka utakuwa kama mwezi mmoja. Mwezi utakuwa kama wiki moja, wiki itakuwa kama siku moja, siku itakuwa kama saa moja na saa itakuwa kama kuchomeka kwa jani la mtende.”[12]

Mambo yametokea kama alivosema. Ambaye atasema kinyume na hayo basi yeye ndiye mwongo mpotevu na anakumbushia wale waliosema:

اللَّـهُمَّ إِن كَانَ هَـٰذَا هُوَ الْحَقَّ مِنْ عِندِكَ فَأَمْطِرْ عَلَيْنَا حِجَارَةً مِّنَ السَّمَاءِ أَوِ ائْتِنَا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ

“Ee Allaah! Kama haya ni haki kutoka Kwako, basi tuteremshie mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo.”[13]

Ni utukufu ulioje wa mafunzo yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´ibaadah alizowafunza Ummah wake! Hakika si vyenginevyo ni haki ya wazi, nuru yenye kung´aa na njia ilionyooka:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ndio njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate vichochoro [vinginevyo]; vikakufarikisheni na njia Yake!”[14]

[1] Ahmad (5/265). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Mishkaah” (5737).

[2] Ibn Hibbaan (361).

[3] 40:78

[4] 6:124

[5] 21:7

[6] 22:52-53

[7] al-Bukhaariy (6632).

[8] 04:64

[9] 09:128

[10] 07:157

[11] 45:18-19

[12] Ahmad (2/537) na Ibn Hibbaan (6842). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Mishkaat” (5448).

[13] 8:32

[14] 06:153

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 73-79
  • Imechapishwa: 14/10/2021