126. Mjadala miezi sita na Abu Haniyfah

al-Qaadhwiy Abu Yuusuf (afk. 182 – Rahimahu Allaah).

157 – Imethibiti kwamba Abu Yuusuf (Rahimahu Allaah) amesema:

”Yeyote mwenye kutafuta dini katika falsafa atakuwa zandiki. Yeyote mwenye kutafuta mali kwa kemia atafilisika. Yeyote mwenye kufuatiliafuatilia maongezi ya kigeni ataongopea.”[1]

 158 – Bashshaar bin Muusa al-Khaffaaf amesema:

”Bishr al-Waliyd al-Kindiy alikuja kwa Abu Yuusuf na kumwambia: ”Unanikataza falsafa wakati ambapo Bishr al-Mariysiy na ´Aliy al-Ahwal wote wawili wanazungumza?” Akasema: ”Wanasema nini?” Wakasema: ”Allaah yuko kila mahali.” Abu Yuusuf akasema: ”Basi  nitawashughulikia.” Walipoletwa kwake mahali alipo, Bishr akasimama na ´Aliy al-Ahwal akasogezwa mbele na mzee mmoja. Abu Yuusuf akamtazama yule mzee na kusema: ”Kama usingelikuwa mtu unayetakiwa kufanyiwa adabu basi ningekuumiza.” Akaamrisha afungwe, akampiga al-Ahwal na akaamrisha azungushwe kati ya watu.”[2]

159 – ´Aliy bin al-Hasan al-Kuraa´iy ameeleza kuwa Abu Yuusuf amesema:

”Nimejadiliana na Abu Haniyfah miezi sita na tukaafikiana juu ya kwamba yeyote mwenye kusema kuwa Qur-aan ni kiumbe ni kafiri.”[3]

160 – Bashshaar al-Khaffaaf ameeleza kuwa amemsikia Abu Yuusuf akisema:

”Yeyote mwenye kusema kuwa Qur-aan ni kiumbe atengwe.”[4]

[1] Ameipokea al-Harawiy katika “Dhamm-ul-Kalaam” (6/104/1) kupitia njia mbili kutoka kwa Abu Yuusuf. Ibn Taymiyyah amethibitisha katika “al-Jawaab al-Faaswil” kuwa ni masimulizi yenye kutoka kwake. al-Harawiy (5/94/2) amepokea mfano wake kutoka kwa Maalik.

[2] Mtunzi ameipokea kupitia kwa Haafidhw Ibn Abiy Haatim: al-Hasan bin ´Aliy bin Mihraan: Bashshaar bin Muusa al-Khaffaaf ametukhabarisha. Bashshaar ni dhaifu na ni mwenye kukosea sana.

[3] Mtunzi ameisimulia kupitia kwa Ibn Abiy Haatim: Ahmad bin Muhammad bin Muslim ametuhadithia: ´Aliy bin al-Hasan al-Kuraa´iy ametuhadithia. Cheni yake ya wapokezi ni nzuri.

[4] Bashshaar ni mnyonge kama ilivyokwishatangulia.

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Uluww lil-´Aliy al-Ghaffaar, uk. 151-152
  • Imechapishwa: 21/07/2024
  • Taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy