12. Sababu ya kuchelewesha swalah wakati wa joto kali

Alama nyingine ya kutukuza amri na makatazo ya Allaah ni kuwa mtu hatokwenda sambamba na ruhusa kwa kupitiliza mpaka, kiasi cha kuwa ni mtu mkavu na asiyesimama juu ya njia ya katikati. Mfano wa hilo ni kuwa Sunnah imekuja kuelezea kuchelewesha swalah ya Dhuhr katika joto kali. Kwa hiyo ruhusa inayopitiliza ni kuichelewesha hadi wakati wa swalah upite au ukaribie kutoka, hapo mtu huyo huwa ametumia ruhusa kupita kiasi. Hekima ya ruhusa hii ni kwamba swalah katika joto kali humzuia mtu kuwa na unyenyekevu na kuhudhurisha moyo na mtu hufanya ´ibaadah kwa machukizo na kuchoka. Basi hekima ya mwekaji Shari´ah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kuwaamrisha waicheleweshe hadi joto lipungue ili mja aswali akiwa na moyo uliohudhuriwa na apate lengo la swalah, ni unyenyekevu na kuelekea kwa Allaah (Ta´ala).

Miongoni mwa hayo pia ni katazo lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuswali wakati chakula kishatengwa au katika hali kuhisi kufanya haja kubwa au haja ndogo, kwa sababu moyo wake unakuwa umegandamana na jambo litakalomvurugia makusudio ya swalah na halitapatikana lengo lake. Basi katika kuelewa kwa mtu katika ´ibaadah yake ni kuangazia jambo lake analohitaji kulimaliza, kisha kuutuliza moyo wake kwa ajili ya swalah na aimalize akiwa moyo wake umeshatulia kwa ajili ya Allaah (Ta´ala), akauelekeza uso wake Kwake na akamuelekea kwa dhati. Rak´ah mbili za swalah ya namna hii ndio mtu husamehewa dhambi zake zilizotangulia. Lengo ni kuwa mtu asichukue ruhusa kwa kupitiliza.

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 30/07/2025