Shaykh Bakr Abu Zayd amesema:

“2- Ngozi ya mwilini mwangu ilisisimka pindi niliposoma kwenye yaliyomo kwenye kitabu chako na kwamba unasema kuwa Sayyid Qutwub anajuzisha kwa asiyekuwa Allaah kuweka Shari´ah. Kitu cha kwanza nilichofanya nilikimbia huko na kuona kuwa inahusiana na nukuu moja katika misitari kadhaa kutoka katika kitabu chake “al-´Adaalah al-Ijtimaa´iyyah”. Niliona kuwa maneno yake hayaafikiani na kichwa cha khabari hichi cha uchokozi. Wacha tuseme kuwa maneno yake kweli yana ibara zisizokuwa wazi na zisizofungamana. Ni vipi mtu anaweza kuyafanya yakawa ni makosa ya kikafiri na kubomoa yote ambayo Sayyid Qutwub (Rahimahu Allaah) amejenga maisha yake juu yake kwa vile alilingania katika Tawhiyd ya Allaah katika hukumu na uwekaji wa Shari´ah na akatupilia mbali sheria za wanaadamu zilizotungwa na akakabiliana na wale wenye kuhukumu kwazo? Hakika Allaah anapenda uadilifu na inswafu katika kila kitu. Sikuonelei isipokuwa – Allaah akitaka – utarejea katika uadilifu na inswafu.”

Mtazame mtu huyu ambaye ametumia sehemu yake kubwa ya maisha katika kuinusuru Sunnah na kuraddi Bid´ah na watu wa Bid´ah na namna ambavyo anasisimka kwa kuwa na ghera juu ya Sayyid Qutwub.

Hata hivyo hakusisimka kwa ghera kwa kukanushwa sifa za Allaah.

Hata hivyo hakusisimka kwa ghera juu ya khaliyfah mwongofu ´Uthmaan bin ´Affaan baada ya Sayyid Qutwub kumtukana kwa dhuluma na kuangusha ukhalifah wake.

Hata hivyo hakusisimka hali ya kuwa na ghadhabu kwa mteuliwa Mtume wa Allaah Muusa (´alayhis-Swalaatu was-Salaam), ambaye Allaah alizungumza nae, baada ya Sayyid Qutwub kumtweza.

Hata hivyo hakusisimka kwa ghera kwa wale Maswahabah aliowatukana kama az-Zubayr, Sa´d na ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf.

Hakusisimka kwa ghera kwa matusi ya Sayyid Qutwub juu ya dola ya Umayyah na kuikufurisha inapokuja katika hukumu na uchumi.

Hakusisimka kwa Takfiyr yake kwa karne nyingi za Ummah.

Ni majanga mangapi alionayo Sayyid Qutwub? Yote haya hayakumtikisa mtu huyu kwa sababu ya ghera yake kwa Sayyid Qutwub.