115 – Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kuyatembelea makaburi kwa ajili ya kupata mazingatio na kukumbuka Aakhirah, kwa sharti kwamba mtu asiseme maneno ya kumghadhibisha Allaah (´Azza wa Jall), kama kumwomba aliyekufa, kuomba msaada kwake pasi po Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kumsifu na kumthibitishia Pepo na mfano wa hayo. Kuna Hadiyth zifuatazo juu ya hilo:

1 – Buraydah bin al-Huswayb (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nilikuwa nimewakatazeni kuyatembelea makaburi, basi sasa yatembeleeni [kwani yanawakumbusha Aakhirah], [na kuyatembelea kwake kuwazidishieni kheri], [basi anayependa kuyatembelea na afanye hivo, lakini msiseme maneno ya upuuzi].”

Ameipokea Muslim (53/6, 6/82), Abu Daawuud (2/72, 131), kupitia mlolongo wake al-Bayhaqiy (4/77), an-Nasaa´iy (1/328, 28, 28, 29, 28, 29, 1/28 330), Ahmad (5/350, 355, 356, 361). Ziada ya kwanza na ya pili ni yake. Abu Daawuud anayo ziada ya kwanza mfano wake, an-Nasaa’iy anayo ziada ya pili na ya tatu.

an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema katika ”al-Majmuu´” (5/310):

”Upuuzi (الهجر) ni maneno ya batili. Makatazo yalikuwa hapo mwanzo kwa sababu ya kuwa bado walikuwa karibu na enzi kabla ya kuja Uislamu. Huenda wakasema maneno ya batili ya zama kabla ya kuja Uislamu. Lakini baada ya Uislamu kuwa thabiti, Shari´ah kuwa imara na alama zake kujulikana sana akawaruhusu kuyatembelea. Lakini akaweka (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tahadhari kwa kusema:

“… wala msiseme maneno ya upuuzi.”

Haifichiki kuwa yale yanayofanywa na watu wa kawaida na wengineo wakati wa matembezi kama kuwaomba waliokufa, kuwaomba msaada na kumuomba Allaah kwa haki ya maiti ni upuuzi mkubwa na maneno batili. Hivyo ni wajibu kwa wanazuoni kubainisha hukumu ya Allaah kuhusu hayo na kuwafundisha watu matembezi kwa mujibu wa Shari´ah na madhumuni yake.”

as-Swan´aaniy amesema katika ”Subul-us-Salaam” baada ya kuleta Hadiyth kuhusu matembezi na hekima yake:

“Yote hayo yanajulisha uwekwaji Shari´ah wa kuyatembelea makaburi na hukumu yake na kwamba ni kwa ajili ya mazingatio. … Ikiwa matembezi hayo hayana sifa hizo, basi yanakuwa si yenye kukusudiwa kwa mujibu wa Shari´ah.”

2 – Abu Sa´iyd al-Khudriy ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nilikuwa nimewakatazeni kuyatembelea makaburi, basi sasa yatembeleeni. Kwani  ndani yake kuna mazingatio. [Wala msiseme maneno yanayomghadhibisha Mola].”

Ameipokea Ahmad (3/38, 63, 66) na al-Haakim (1/374-375), kutoka kwake na al-Bayhaqiy (4/77), ambaye amesema: ”Swahiyh kwa mujibu wa masharti ya Muslim” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye, na mambo ni kama alivosema. Ameipokea vilevile al-Bazzaar. al-Haythamiy amesema katika ”al-Majma´” (3/58):

”Cheni yake wanaume wake ni wanaume wa Swahiyh.”

Mfano wake iko kwa Ahmad pia kupitia njia nyingine. Cheni yake ya wapokezi ni nzuri katika ufuatiliaji. Kuna nyingine inayoitia nguvu kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr kwa tamko la al-Bazzaar. Ameipokea at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam as-Swaghiyr” na wapokezi wake ni wenye kuaminika.

3 – Anas bin Maalik ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Nilikuwa nimewakatazeni kuyatembelea makaburi. Basi yatembeleeni, kwani yanalainisha mioyo, kufanya macho kutokwa na machozi na kuwakumbusheni Aakhirah. Msiseme maneno ya upuuzi.”

Ameipokea al-Haakim (1/376) kwa cheni ya wapokezi nzuri. Kisha akaipokea tena (1/375, 376), Ahmad (3/237, 250) kwa njia nyingine yenye tamko kama hilo, lakini ndani yake kuna udhaifu.

Katika mlango huu kuna Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh), ambayo itakuja baadaye.

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 226-229
  • Imechapishwa: 03/08/2026