117. Ahl-us-Sunnah tunaangalia hoja, Ahl-ul-Bid´ah wanaangalia msemaji

Maoni haya yametumiwa vibaya na watu wa Bid´ah ambapo wakayafanya ni kisingizio cha kuipiga vita Sunnah na wamejitetea kwa maneno ya Shaykh na mwanafunzi wake dhidi ya wanusuraji na wenye kufuata Sunnah. Wazushi hao wa Sunnah hawajui au wamejifanya eti hawajui kwamba wafuasi wa Sunnah hawamuigizi mtu yeyote katika dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kama wanavyofanya hao. Hawatoi kipaumbele kauli ya mwanachuoni yeyote juu ya ukweli uliobainishwa kwao, pasi na kujali mwanachuoni huyo ni mwema kiasi gani katika elimu na wema wake. Wao huangalia dalili – si jina la msemaji – hali ya kujikita katika maneno ya Imaam wa Maalikiy (Rahimahu Allaah):

“Hakuna yeyote miongoni mwetu isipokuwa anakataliwa na kukubaliwa maneno yake, isipokuwa bwana mwenye kaburi hili.”

Amesema tena:

“Kila mmoja maneno yake yanachukuliwa na kurudishwa nyuma, isipokuwa bwana mwenye kaburi hili.”

Ikiwa inakubaliwa na wanazuoni kwamba kila ´Aqiydah au maoni mtu anayoibeba katika maisha ina athari katika mwenendo wake – ikiwa ni nzuri au mbaya – basi ni sahihi pia kusema kuwa athari humwonyesha aliyesababisha. Kwa hivyo hatuna shaka yoyote kwamba kauli hii ina athari mbaya kwa mwenye kuishikilia. Mfano wa hilo mtu hatakuwa na bidii ya kutafuta thawabu na daraja za juu kwa juhudi zake, kwa sababu anajua kuwa watu humletea thawabu mara mia kwa siku kwa waislamu wote walioko hai na waliokufa – naye ni mmoja wao – basi kwa nini asijitume mwenyewe? Je, huoni mfano wa baadhi ya Mashaykh wanaoishi kutokana na juhudi za wanafunzi wao, hawajitahidi wao wenyewe kutafuta chakula chao kwa jasho lao na juhudi zao. Sababu yake ni kuwa wametegemea kazi ya wengine. Huu ni mfano wa kilimwengu na unafahamika pia kiroho, kama ilivyo katika suala hili. Laiti kwamba jambo hili lingeishia hapo tu, bali lina athari nyingine kubwa zaidi. Mfano wa maoni yanayosema kwamba hajj inajuzu kufanywa kwa niaba ya mtu mwingine hata kama hakuwa na udhuru – kama matajiri wengi wanaokosa wajibu huu. Maoni haya huwafanya watu wazembee na wasikuwe na bidii juu ya hajj na huku wakisema mioyoni mwao:

“Watanifanyia hajj baada ya kifo changu.”

Bali kuna madhara zaidi ya hayo, kama maoni yanayosema kuwa swalah haitalazimika tena kwa mfu aliyekuwa haswali. Hili ni miongoni mwa sababu za baadhi ya waislamu kuacha swalah, kwa sababu wanategemea kuwa watu watawaswalia baada ya kufa kwao. Yapo maono mengine mengi ambayo athari yake ni dhahiri kwa jamii.

Kwa hivyo ni wajibu kwa mwanachuoni mwenye nia ya marekebisho kupinga na kuyatupilia mbali maoni haya, kwa sababu zinapingana na maandiko ya Shari´ah na madhumuni yake mema. Linganisheni athari za maoni haya na athari za wale wanaoshikamana na maandiko bila ya kutoka nje yake kwa tafsiri wala kipimo ambapo mtapata tofauti kama mchana na usiku. Kwa sababu yule asiyechukua kauli hizo za juu, hawezi kutegemea thawabu ya wengine, kwani anaamini kuwa hatasalimika isipokuwa kwa matendo yake mwenyewe na hana thawabu isipokuwa kwa kile alichokitenda mwenyewe. Bali ni wajibu kwake kujitahidi kadiri awezavyo mpaka aache athari njema nyuma yake atakayopewa thawabu wakati akiwa peke yake kaburini badala ya zile thawabu za kuhurumiwa. Hili ni miongoni mwa sababu nyingi zilizosababisha Salaf kusonga mbele na sisi kubakia nyuma, Allaah akawanusuru na sisi akatukosesha nusura. Namwomba Allaah (Ta´ala) atuongoze kama alivyowaongoza, atunusuru kama alivyowanusuru.

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 221-223
  • Imechapishwa: 03/08/2026