Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

92 – ´Arshi na Kursiy ni haki.

MAELEZO

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameumba mbingu, ardhi, Kursiy na ´Arshi. Vyote hivyo ni viumbe vya Allaah (´Azza wa Jall). Mbingu ziko juu ya ardhi, bahari iko juu ya mbingu, juu ya bahari kuna Kursiy na juu ya Kursiy kuna ´Arshi. Kwa hivyo ´Arshi ndio kiumbe kilicho juu zaidi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hazikuwa mbingu saba ukilinganisha na Kursiy isipokuwa ni kama dirhamu saba zilizowekwa kwenye ngao ya vita. Kursiy ukiilinganisha na ´Arshi si kitu isipokuwa ni kama mfano wa kijipete cha chuma kilichotupwa katika uwanja mkubwa.”[1]

Zinalingana nini dirhamu saba zilizowekwa katika ngao ya vita? Allaah (Ta´ala) amesema kuhusiana na hilo:

وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ

“Wala hawakizunguki chochote katika elimu Yake isipokuwa kwa akitakacho. Kursiy Yake imeenea mbingu na ardhi.”

´Arshi ni kubwa zaidi kuliko Kursiy. Kursiy ukiilinganisha na ´Arshi ni kama mfano wa kijipete cha chuma kilichotupwa katika uwanja mkubwa. Kijipete hichi kinalingana nini katika ardhi kubwa? Si chochote. Viumbe hivi vikubwa na vipana hakuna anayejua ukubwa wavyo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). ´Arshi ndio kiumbe kilicho juu zaidi, na Allaah (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi Yake na juu ya viumbe Wake wote.

[1]Ibn Abiy Shaybah katika ”Kitaab-ul-´Arsh” (58), Ibn Hibbaan (361), Abuush-Shaykh (259) na wengineo. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (109).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 123-124
  • Imechapishwa: 10/11/2024