Wanafanya hivo bila pasi na upotoshaji. Upotoshaji maana yake ni kuyapotosha maneno, inafanywa hivo ima kwa kuzidisha au kwa kupunguza.

Wanafanya hivo pasi na kuzikanusha sifa. Maana yake ni kuikanusha sifa, kukengeusha au kupindisha maana yake.

Wanafanya hivo bila pasi na kuzifanyia namna. Kwa mfano hawasemi “Allaah amelingana namna hii”, “Allaah hushuka namna hii” au kwamba “Allaah hukasirika namna hii”.

Wanafanya hivo bila pasi na kufananisha. Hawasemi “Allaah hukasirika mfano wa hivi”, “Allaah amelingana mfano wa hivi”, “Allaah husikia mfano wa hivi”, “Allaah huona mfano wa hivi”.

Badala yake wanamthibitishia Allaah majina na sifa zake kwa njia inayolingana Naye. Hawabadilishi, hawapotoshi, hawampigiii mfano, hawakanushi na hawamfanyii namna. Kanuni yao katika hilo ni ifuatayo:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

Wakati Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) na wengineo katika Salaf walipoulizwa juu ya hili  wakasema:

“Kulingana kunajulikani. Namna haijulikani. Kuamini hilo ni wajibu. Kuuliza juu ya hilo ni Bid´ah.”[1]

Bali Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ni mwenye kuelezwa kwa sifa, kama alivyojieleza Mwenyewe, bila ya kuzidisha wala kupunguza. Nazo ni sifa za kikweli. Kulingana ambako ni kwa hakika. Kusikia kwa hakika. Kuridhia kwa hakika. Kukasirika kwa hakika. Sifa zote hazina mafumbo. Bali ni za hakika kwa njia inayolingana na Allaah.

Hatuziwekei namna na kuzipigia mfano, hatuzishabihishi wala kuzipotosha. Bali tunazipitisha kama zilivyo dhahiri yake. Kila kilichothibiti ndani ya Qur-aan na Sunnah tunakipitisha kama kilivyokuja. Kama walivyosema Salaf:

“Zipitisheni kama zilivyokuja.”[2]

Bila ya kuzipotosha, kuzikanusha wala kuzipindisha maana. Tunazipitisha na wakati huohuo tunaamini kuwa ni za haki na kwamba ni sifa zenye kuthibiti na kwamba Allaah anasifika nazo kihakika. Tunafanya hivo bila ya kushabihisha, kufananisha, kuziwekea namna wala kuzipotosha. Namna hii ndivyo walivyosema Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

[1] Masimulizi haya yamepokelewa na Salaf wengi. Miongoni mwao ni Imaam Maalik, mwalimu wake Rabiy´ah bin Abiy ´Abdir-Rahmaan, Imaam ash-Shaafi´iy, al-Awzaa´iy, ath-Thawriy na wengineo.

[2] al-Khallaal katika “as-Sunnah” (01/243), al-Aajurriy katika “ash-Shariy´ah” (720), “at-Tawhiyd” (794) (03/307), al-Lalakaa´iy katika “Sharh ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah” (930) (03/527), asw-Swaabuuniy katika “´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth” (249).

 

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 17-19
  • Imechapishwa: 17/10/2024