Imepokelewa katika Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa ameueleza mwezi wa Ramadhaan kuwa ni mwezi uliyobarikiwa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Umekujieni mwezi wa Ramadhaan – ni mwezi wenye baraka. Allaah amekufaradhishieni kufunga. Ndani yake milango ya Pepo hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan waovu hutiwa pingu.”[1]

Tunacholenga katika Hadiyth ni pale ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameusifu mwezi wa Ramadhaan kuwa ni wenye baraka. Baraka za mwezi huu zinakusanya vipindi vyake vyote na kila saa, kuanzia mwanzo wa kuingia kwake mpaka kutoka kwake. Vipindi vyake vyote vimebarikiwa. Ndani yake kuna baraka, kheri nyingi na fadhilah nyingi.

Miongoni mwa baraka za mwezi huu ni yale aliyoeleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth hii ya kuwa inafunguliwa milango ya Pepo, inafungwa milango ya Moto na mashaytwaan waovu wanatiwa pingu. Baraka hizi ni maalum juu ya mwezi huu pekee. Ni baraka ambazo hazipatikani katika miezi mingine. Milango yote ya Pepo inafunguliwa na huafungwi mlango wowote. Milango yote ya Moto inafungwa na haufunguliwi mlango wowote. Mashaytwaan waovu wanafungwa na hakuna yeyote katika wao anayeweza kumvamia yeyote kama walivokuwa wanaweza kufanya katika miezi mingine. Zote hizi ni baraka tukufu ambazo zinaamsha hima, maazimio na kuwapa uchangamfu watu kumwelekea Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

[1] Ahmad (7148) na an-Nasaa´iy (2106) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 13/04/2022