11. Mtu anayetengeneza masanamu na kuyajengea makaburi

Swali 11: Unasemaje juu ya ambaye anasimamisha masanamu, vibanda vya mazishi, makaburi na anajenga misikiti juu yake na sehemu za ´ibaadah juu yake, kisha akatenga watu na mali kwa ajili ya hayo, akaweka taasisi zinazoyasimamia, akawaruhusu watu kuyaabudu, kuyazunguka kwa kutufu, kuyaomba na kuchinja kwa ajili yake?

Jibu: Huyu ni mshirikina. Tunamuomba Allaah salama na hifadhi. Yeyote anayesimamisha masanamu ni mshirikina. Ukiongezea juu ya hayo ikiwa atatenga mali na mali zisizohamishika kwa ajili yake au akayatetea, basi pia anakuwa kafiri na mwenye kuzuia watu wasifuate njia ya Allaah. Hivyo mtu huyu amekusanya aina mbili za ukafiri:

1 – Amefanya kitendo cha ukafiri yeye mwenyewe.

2 – Amezuilia watu kufuata dini ya Allaah.

Huyu ni miongoni mwa wale waliotajwa katika maneno Yake Allaah:

الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ زِدْنَاهُمْ عَذَابًا فَوْقَ الْعَذَابِ بِمَا كَانُوا يُفْسِدُونَ

“Wale waliokufuru na wakazuia kutokana na njia ya Allaah, tutawazidishia adhabu juu ya adhabu kwa sababu ya ufisadi waliokuwa wakiufanya.”[1]

Huyu ni miongoni mwa wenye kueneza maharibifu katika ardhi. Amekufuru yeye mwenyewe na amewazuia watu wasifuate dini ya Allaah. Tunamuomba Allaah atupe usalama.

[1] 16:88

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah wa Ajwibah fiy-Iymaan wal-Kufr, uk. 30
  • Imechapishwa: 05/01/2026