11. Mfumo wa Salaf mpaka siku ya Qiyaamah

Hili ndio la wajibu juu ya kila kitu na khaswa katika majina na sifa za Allaah, majina na sifa za Allaah ni kitu maalum kutokana na umuhimu wake kwa vile watu wameyaingilia. Kwa hivyo sisi tunasema juu yake yale aliyosema Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah zake – ambao ndio wanafunzi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na wale waliowafata kwa wema. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia mwanzoni ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”

Muhaajiruun ni wale waliohama wakaelekea Madiynah na kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Waliiacha miji, mali zao na watoto wao kwa ajili ya kuisalimisha dini na kumnusuru Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maswahabah bora ni Muhaajiruun. Walihama kwa ajili ya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Je, kuna kujitolea kukubwa baada ya hili? Hakuna.

Kisha wanafuatia Answaar ambao walijitolea na kunusuru. Waliifungua miji na nyumba zao na nyoyo zao kwa ajili ya ndugu zao Muhaajiruun na wakakabiliana nao kwa maliwazo na mapenzi. Wana fadhilah yao baada ya Muhaajiruun, kwa sababu ni wanusuraji wa Allaah, Mtume Wake na waumini. Allaah (Ta´ala) amesema juu yao:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

”Na wale waliokuja baada yao wanasema: ”Ee Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[1]

Hawa ndio Answaar.

وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍُ

“… na wale waliowafuata kwa wema… ”

Bi maana vile vizazi vya wale wataokuja baada ya Muhaajiruun na Answaar mpaka siku ya Qiyaamah. Lakini zingatia Allaah amelifungamanisha hilo kwa wema. Kwa sababu baadhi ya watu husema kuwa wanawafata Muhaajiruun na Answaar pasi na kujua ni vipi. Ima wakaingia katika upetukaji mipaka na wakavuka mipaka katika mfumo wao, au wakazembea na kupunguza. Ndio maana Allaah akawataja wale wanaowafata kwa wema, bi maana wanamairi mfumo wa Muhaajiruun na Answaar pasi na kuchupa mipaka na kuzembea.

[1] 59:10

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 25/07/2024