11. Hakuna anayefanya kitu bila idhini ya Allaah

54 – Tambua ya kwamba wadudu, wanyama wakali na wanyama wote wanaotambaa kama vile sisimizi, nzi na mchwa, wameamrishwa. Hawafanyi kitendo chochote isipokuwa kwa idhini ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

55 – Inatakiwa kuamini kuwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) tokea mwanzo aliyajua yote yaliyokuwepo na ambayo hayakuwepo na yaliyoko. Hakika Allaah ameyadhibiti na kuyahesabu kwelikweli. Mwenye kusema kwamba hayajui yaliyokuwepo na yatayokuwepo, basi amemkufuru Allaah Mtukufu.

56 – Hakuna ndoa isipokuwa kwa kuwepo walii, mashahidi wawili waadilifu na mahari, ni mamoja yawe madogo au makubwa. Asiyekuwa na walii, basi mtawala ndiye anakuwa walii wake.

57 – Mwanaume anapomtaliki mwanamke mara tatu, basi anakuwa haramu kwake na hawi halali kwake mpaka aolewe na mume mwengine.

58 – Haijuzu kuimwaga damu ya muislamu ambaye anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni mja na Mtume wa Allaah isipokuwa kwa moja katika mambo matatu: mwenye kuzini baada ya kuingia ndani ya ndoa, mwenye kuritadi baada ya kuamini au mwenye kuua nafsi ya muumini pasi na haki. Anapaswa kuuawa kwa ajili ya haya. Mbali na mambo haya, damu ya muislamu juu ya muislamu mwenzake ni haramu milele mpaka Qiyaamah kisimame.

59 – Kila kitu alichokiwajibishia Allaah kutoweka, basi kitatoweka – isipokuwa Pepo, Moto, ´Arshi, Kursiy, Ubao, Kalamu na Parapanda. Hakuna kitu katika hivi kitachotoweka. Baada ya hapo Allaah atawafufua viumbe siku ya Qiyaamah katika ile hali waliyofia. Atawafanyia hesabu vile Anavyotaka. Kundi moja litaingia Peponi na kundi lingine litaingia Motoni. Aidha Atawaambia viumbe vyengine vilivyobakia ambavyo havikuumbwa kwa ajili ya kubaki: “Kuweni udongo!”

  • Mhusika: Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin Khalaf al-Barbahaariy (kfk. 329)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh-us-Sunnah, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 17/12/2024