Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

90 –Hayo ni katika mafundo ya imani, misingi ya utambuzi na kutambua upwekekaji wa kuabudiwa kwa Allaah (Ta´ala) na uola Wake. Kama alivosema (Ta´ala) ndani ya Kitabu Chake:

وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا

”Ameumba kila kitu kisha akakikadiria kipimo sawasawa.”[1]

وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ قَدَرًا مَّقْدُورًا

“Na amri ya Allaah daima ni makadirio yaliyokadiriwa.”[2]

MAELEZO

Kuamini makadirio ni katika kumwamini Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Yule asiyeamini mipango na makadirio ya Allaah basi hamwamini Allaah (Jalla wa ´Alaa). Bali anakuwa amemfanya Allaah (´Azza wa Jall) kuwa na mapungufu. Kuamini makadirio ni katika mambo ya ´Aqiydah na si katika mambo ya yanayochukua nafasi ya pili au mambo ya matawi. Kuamini mipango na makadirio ya Allaah ni miongoni mwa misingi ya ´Aqiydah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na kuamini Qadar, kheri na shari yake.”[3]

Kuamini mipango na makadirio ya Allaah kunaingia katika kuamini uola wa Allaah kwa sababu inahusiana na matendo ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Yule mwenye kupinga mipango na makadirio ya Allaah hawi mwenye kuamini uola wa Allaah.

وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا

”Ameumba kila kitu kisha akakikadiria kipimo sawasawa.”

وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ قَدَرًا مَّقْدُورًا

“Na amri ya Allaah daima ni makadirio yaliyokadiriwa.”

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

”Hakika kila kitu Sisi Tumekiumba kwa makadirio.”[4]

Aayah hizi tatu, na nyenginezo, zinafahamisha juu ya kuamini mipango na makadirio ya Allaah:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hausibu msiba wowote [kukupateni] isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Yeyote   anayemuamini Allaah, basi huuongoza moyo wake. – Allaah kwa kila kitu ni mjuzi.”[5]

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا

 “Hakuna msiba wowote unaokusibuni katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla Hatujauumba.”[6]

Bi maana Ubao uliohifadhiwa.

[1]25:2

[2]33:38

[3] Muslim (8).

[4]54:49

[5]64:11

[6]57:22

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 121-122
  • Imechapishwa: 06/11/2024