Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Karne bora ni ya wale waliomuona na wakamuamini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kisha ile itakayofuatia, kisha ile itakayofuatia.

MAELEZO

Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba wanaamini kwamba bora ya karne ya Ummah ni Maswahabah. Maswahabah ni wale waliokutana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakamwamini na wakafa hali ya kuwa ni waumini. Yule mwenye kumwamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kukutana naye sio Swahabah; kama mfano wa wanafunzi wa Maswahabah (Taabi´uun). Vilevile ni sharti mtu aendelee juu imani mpaka pale atakapofariki ili kuzingatiwa kuwa Swahabah. Yule mwenye kuritadi anazingatiwa ni murtadi na sio Swahabah. Ni lazima yatimie masharti haya matatu ili mtu azingatiwe kuwa ni Swahabah:

1 – Akutane na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), haijalishi kitu kumerefuka au kufupika kutangamana naye.

2 –  Amwamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa kukutana naye.

3 – Afe hali ya kuwa ni muumini.

Maswahabah ndio karne bora. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewashuhudilia jambo hilo na kusema:

“Watu bora ni wa karne yangu. Kisha wale watakaofuatia, kisha wale watakaofuatia.”[1]

Baada ya Maswahabah wanafuatia wanafunzi wa Maswahabah na baada yao wanafuatia wanafunzi wa wanafunzi wa Maswahabah. Hawa ndio watu bora wa Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya hapo bora ya watu ni wale wenye kuwaigiliza. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia mwanzoni ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[2]

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao ni wenye kusema: “Mola wetu!Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo kwa wale walioamini – Mola wetu! Hakika ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[3]

[1] al-Bukhaariy (2652) na Muslim (2533).

[2] 09:100

[3] 59:10

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 82
  • Imechapishwa: 02/09/2021