Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Fikira yao inapelekea kwamba Qur-aan sio mwongozo kwa watu, ubainifu, ponyo kwa yale yaliyomo vifuani, nuru wala marejeo wakati wa magomvi. Ukweli wa mambo ni kuwa watu hawa wenye kujikakama wanaona kuwa Qur-aan na Sunnah havifahamishi ´Aqiydah yoyote ambayo ni lazima kuiamini.

MAELEZO

Yule anayetaka tuhukumu kwa akili, mantiki na fikira, maana yake ni kuwa Qur-aan sio kama alivyoisifu Allaah, ya kwamba ni mwongozo kwa watu. Bali imekuja kupofusha na kupotosha. Haki ni kwamba Allaah ameiteremsha Qur-aan ili iwe ni mwongozo. Hakuna kitu kinachotatua mizozo kati ya watu isipokuwa tu Qur-aan. Kuhusu akili, fikira na maoni havifumbui migogoro, kwa sababu kila mmoja ana maoni yake aliyoyashikilia. Kisha kunakuja msemo kwamba nisije na nikakulazimisha maoni yangu. Ni kweli kwamba sintokuja nikakulazimisha maoni yangu, lakini nakulazimisha Wahy ambao ndio unaotakiwa kumuhukumu kila mmoja. Tukirejea katika maoni, kila mmoja atamwambia mwenzie kwamba asimlazimishe maoni yake. Lakini tukisema kuwa marejeo yanatakiwa kuwa Qur-aan, mizozo na magomvi yanamalizika. Kwa ajili hiyo utawaona wako katika hali ya fujo. Mizozo inayokuwa kati yao haimaliziki. Sambamba na hilo utawaona Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni ndugu wanaopendana – himdi zote njema anastahiki Allaah. Hakuna kati yao shida wala tofauti kwa sababu wanahukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hivyo zingatia tofauti kati ya hawa na hawa. Fikira hii inapelekea kwamba mizozo na tofauti hazitakiwi kurejeshwa katika Qur-aan na Sunnah kwa sababu sio mwongozo na nuru na wala havitatui migogoro.

Maneno yake Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ”fikira yao” anamaanisha fikira ya Mu´attwilah, inayosema kuwa utambuzi wa majina na sifa za Allaah hauchukuliwi kutoka katika Qur-aan na Sunnah, bali unachukuliwa kutoka katika dalili za kiakili na hoja za kiyakini. Kwa mujibu wa fikira hii ni kwamba ilikuwa bora zaidi kuwaacha watu pasi na Qur-aan na Sunnah. Muda wa kuwa akili na falsafa inatosha, basi uwepo wa Qur-aan na Sunnah hauna maana yoyote. Namna hii ndivo inavyopelekea fikira yao, kwa sababu wako na yenye kuwatosheleza katika fikira, akili na mawazo yao. Tunajua fika kuwa fikira yao inapelekea kuwa Qur-aan na Sunnah si dalili wala hukumu yoyote, kwa sababu mantiki, falsafa na mjadala vinatosheleza.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 156-157
  • Imechapishwa: 04/09/2024