107. Kijana chipukizi anatakiwa kuchukua msimamo gani juu ya mapote ya leo?

Swali 107: Kijana chipukizi anatakiwa kuchukua msimamo gani juu ya mapote yaliyopo leo ambayo yanataka ajiunge nayo?

Jibu: Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wametueleza kuwa yatazuka mapote yanayoenda kinyume na njia ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na wakatubainishia ni namna gani tutataamiliana nayo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Kwamba hii ni njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate njia za vichochoro nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo alivyokuusieni kwayo mpate kumcha.” [1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amelibainisha hilo ubainifu wa wazi. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituchorea ardhini msitari ulionyooka kisha akasema: “Hii ni njia ya Allaah.” Kisha akachora mistari mingi kuliani na kushotoni na kusema: “Hivi ni vijia. Katika kila njia yupo shaytwaan anayelingania kwayo.” Halafu akasoma:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ndio njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate vichochoro [vinginevyo]; vikakufarikisheni na njia Yake!”[2]

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Watu walikuwa wakimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu mambo ya kheri na mimi nikimuuliza kuhusu mambo ya shari kwa kuchelea yasije kunipata. Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tulikuwa katika kipindi cha kikafiri na shari na Allaah akatuletea kheri hii. Je, kuna shari baada ya kheri hii?” Akajibu: “Ndio.” Nikasema: “Je, kuna kheri baada ya shari hiyo?” Akajibu: “Ndio, na itakuwa na moshi.” Nikamuuliza: “Ni upi moshi wake?” Akajibu: “Ni watu wenye kufuata isiyokuwa njia na uongofu wangu. Kuna mambo utayokubaliana nayo na mengine utayapinga.” Nikasema: “Kuna shari baada ya kheri hiyo?” Akasema: “Ndio, fitina ya upofu na walinganizi katika milango ya Motoni. Yule mwenye kuwaitikia wanamtupa humo.” Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tueleze nao.” Akasema: “Ni watu wanaotokamana na sisi na wanazungumza lugha yetu.” Nikauliza: “Unaniamrisha nini nikikutana na hilo?” Akasema: “Shikamana na mkusanyiko wa waislamu na kiongozi wao.” Nikasema: “Vipi kukiwa hakuna mkusanyiko wala kiongozi?” Akasema: “Jiepushe na hayo makundi yote hata kama utahitajia kuuma mzizi wa mti mpaka yakufikie mauti.”[3]

Kwa maana hiyo ni lazima kwa vijana na wengine kuyakataa makundi na mapote yote yanayotofautiana na Ahl-us-Sunnah na wanyookaji, atahadhari kutokana na walinganizi wanaolingania katika makundi hayo, kama ambavyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha nayo, na sambamba na hilo alazimiane na Ahl-us-Sunnah. Ahl-us-Sunnah ndio kundi pekee lililothibiti juu ya yale aliyokuwemo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake, kwa sababu wanatendea kazi maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hakika yule katika nyinyi atakayeishi kipindi kirefu basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza. Ziumeni kwa magego yenu. Na nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotofu.”[4]

Akaamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa kutofautiana kushikamana barabara na Sunnah zake na Sunnah za makhaliyfah wake waongofu na kulazimiana na mkusanyiko wa waislamu na kiongozi wao.

[1] 6:153

[2] an-Nasaa’iy (6/343), Ahmad (1/435), ad-Daarimiy (202) na al-Bazzaar (57113).

[3] al-Bukhaariy (3606) na Muslim (1847).

[4] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 250-252
  • Imechapishwa: 18/08/2024
  • Taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy