106. Swawm ya Ramadhaan imemalizika, lakini ´ibaadah ya swawm inaendelea

Ndugu zangu! Ingawa umemalizika mwezi wa Ramadhaan lakini itambulike kuwa matendo ya muumini hayamalizika kabla ya yeye kufa. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ

“… na mwabudu Mola wako mpaka kikufikie kifo.”[1]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

“Enyi walioamini! Mcheni Allaah ukweli wa kumcha na wala msife isipokuwa nyinyi ni waislamu.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapokufa mja ndipo matendo yake hukatika.”

Kwa hivyo kifo ndio kimefanywa kuwa kikomo cha kukatika kwa matendo. Ingawa imekatika funga ya Ramadhaan hata hivyo muumini hakatishi ´ibaadah ya swawm. Swawm bado ni yenye kuendelea kusuniwa mwaka mzima. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Ayyuub al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayefunga Ramadhaan kisha akaifuatishia [siku] sita za Shawwaal, basi anakuwa kama amefunga mwaka mzima.”

Kuna swawm nyingine ambayo ni kufunga siku tatu kila mwezi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Kufunga siku tatu kila mwezi na Ramadhaan moja hadi nyingine hiyo ni swawm ya mwaka mzima.”

Ameipokea Ahmad na Muslim.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ameniusia kipenzi mwandani wangu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mambo matatu” ambapo akataja moja wapo “kufunga siku tatu kila mwezi.”

Bora zaidi siku tatu hizo iwe yale masiku meupe; tarehe 13, 14 na 15. Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Ee Abu Dharr! Utapofunga siku tatu katika mwezi basi funga kumi na tatu, kumi na nne na kumi na tano.”

 Ameipokea Ahmad na an-Nasaa´iy katika “as-Swahiyh” yake.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu swawm ya siku ya ´Arafah ambapo akasema:

“Inasamehe mwaka uliopita na mwaka ujao.”

Aliulizwa kuhusu kufunga ´Aashuuraa´ ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Inasamehe mwaka uliopita.”

Aliulizwa kuhusu kufunga siku ya jumatatu ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hiyo ni siku niliyozaliwa na siku niliyotumilizwa au kuteremshiwa.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa:

“Ni swawm ipi ambayo ni bora baada ya mwezi wa Ramadhaan?” Akasema: “Swawm bora baada ya mwezi wa Ramadhaan ni funga ya mwezi wa Allaah Muharram.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Sijapatapo kumuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akikamilisha mwezi wowote isipokuwa mwezi wa Ramadhaan. Sijapatapo kumuona akifunga kwa wingi mwezi wowote kama Sha´baan.”

Imekuja katika tamko jengine:

“Alikuwa akiufunga isipokuwa siku chache tu.”

Amesimulia tena (Radhiya Allaahu ´anhaa):

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi kufunga jumatatu na alkhamisi.”

Wameipokea watano isipokuwa Abu Daawuud ambaye yeye ameipokea kupitia kwa Usaamah bin Zayd.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Matendo hudhihirishwa siku ya jumatatu na alkhamisi na kwa hivyo napenda matendo yangu yaonyeshwe hali ya kuwa nimefunga.”[3]

Ameipokea at-Tirmdhiy.

[1] 15:99

[2] 03:102

[3] Dhaifu lakini kuna nyingine inayoitolea ushahidi na kuipa nguvu. Imethibiti katika “as-Swahiyh” ya Muslim kwamba matendo yanaonyeshwa kila siku ya jumatatu na alkhamisi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 226-228
  • Imechapishwa: 01/04/2024