Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

87 – Wino wa kalamu umekauka kwa yatayotokea mpaka siku ya Qiyaamah. Yale yaliyomkosa mja, hayakuwa yenye kumpata, na yale yaliyompata hayakuwa yenye kumkosa.

MAELEZO

Hii ndio maana ya kuamini mipango na makadirio. Unatakiwa kutambua kuwa hakuna kitachokupata isipokuwa kile ambacho Allaah amekuandikia kikupate, na yale yaliyokupata hayakuwa yenye kukukosa, na yale yaliyokukosa hayakuwa yenye kukupata.

Ukikupata msiba ambao unauchukia, basi unatakiwa kujua kuwa umekwishaandikwa katika Ubao uliohifadhiwa na ni lazima ukupate. Kufikiria hivo kunakuwaliwaza na hivyo hukati tamaa wala hukasiriki. Hivyo unamuamini Allaah (´Azza wa Jall).

Yale yaliyokukosa hayakuwa yenye kukupata ijapo utafanya kila uliwezalo ili yaweze kukupata. Iwapo utapambana kukifikia kitu na ukatumia nguvu na jitihada zako zote basi hutofanikiwa. Kwa hivyo ukishafanya sababu na ukapambana nguvu na jitihada zako zote pasi na kufanikiwa,  basi unatakiwa kujisalimisha na uamini mipango na makadirio. Usifadhaike. Usiwe na wasiwasi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pupia juu ya yale yanayokunufaisha na mtake msaada Allaah na wala usivunjike moyo. Utapofikwa na jambo usiseme ´Lau ningelifanya hivi basi ingelikuwa kadhaa na kadhaa´. Lakini badala yake sema:

قَدَراللهوماشاءفعل

“Hivi ndivyo alivyokadiria Allaah na hufanya atakavyo.”

Kwani hakika ya ´lau` hufungua matendo ya shaytwaan.”[1]

Ukiyajua haya basi mambo yatakuwa mepesi kwako. Usivunjike moyo na wala kukata tamaa. Mambo yote yako mikononi Mwake (Subhaanah). Ni kweli kwamba unatakiwa kufanya sababu na kupupia yale yenye kukunufaisha, lakini matokeo yanatokana na Allaah (´Azza wa Jall). Isitoshe wewe hujui kheri ni ipi kwako? Huenda Allaah (´Azza wa Jall) amekunyima kitu fulani kwa sababu endapo ungekipata pengine kikawa na madhara kwako. Allaah anajua na wewe hujui. Kwa hiyo ni lazima kwako kuridhia mipango na makadirio ya Allaah. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

قُل لَّن يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَنَا

“Sema: “Halitusibu lolote isipokuwa lile alilotukidhia Allaah.”[2]

Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ كَفَرُوا وَقَالُوا لِإِخْوَانِهِمْ إِذَا ضَرَبُوا فِي الْأَرْضِ أَوْ كَانُوا غُزًّى لَّوْ كَانُوا عِندَنَا مَا مَاتُوا وَمَا قُتِلُوا لِيَجْعَلَ اللَّـهُ ذَٰلِكَ حَسْرَةً فِي قُلُوبِهِمْ ۗ وَاللَّـهُ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

“Enyi walioamini! Msiwe kama wale waliokufuru na wakasema kuhusu ndugu zao waliposafiri katika ardhi au walipokuwa vitani: “Lau wangelikuwa kwetu basi wasingelikufa na wala wasingeliuawa, ili Allaah afanye hayo kuwa ni majuto kwenye nyoyo zao; na Allaah anahuisha na anafisha; na Allaah anayaona vyema myatendayo.”[3]

قُل لَّوْ كُنتُمْ فِي بُيُوتِكُمْ لَبَرَزَ الَّذِينَ كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقَتْلُ إِلَىٰ مَضَاجِعِهِمْ

“Sema: “Lau mngelikuwa majumbani mwenu, bila shaka wangejitokeza wale walioandikiwa kuuwawa kwenye mahali pa kuangukia wafe.”[4]

قُل لَّوْ كُنتُمْ فِي بُيُوتِكُمْ لَبَرَزَ الَّذِينَ كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقَتْلُ إِلَىٰ مَضَاجِعِهِمْ

“Sema: “Lau mngelikuwa majumbani mwenu, bila shaka wangejitokeza wale walioandikiwa kuuwawa kwenye mahali pa kuangukia wafe.”[5]

Yale ambayo mtu ameandikiwa ni lazima yampate hata kama atafanya kila aliwezalo ili kujilinda kutokamana nayo. Hakuna awezaye kumlinda kutokamana na mipango na makadirio ya Allaah:

أَيْنَمَا تَكُونُوا يُدْرِككُّمُ الْمَوْتُ وَلَوْ كُنتُمْ فِي بُرُوجٍ مُّشَيَّدَةٍ

“Popote mtakapokuwa yatakufikieni mauti, japo mkiwa katika ngome zilizo na nguvu.”[6]

[1] Muslim (2664).

[2]9:51

[3]3:156

[4]03:15

[5]03:154

[6]4:78

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 118-119
  • Imechapishwa: 05/11/2024