Aswali kwa unyenyekevu na kwa kuuhudhurisha moyo. Amtaje na kumuomba Allaah kwa wingi na ataraji rehema za Allaah na kuogopa adhabu Yake. Aidha kile kitendo cha watu kukusanyika katika uwanja mmoja kwa ajili ya kuswali swalah ya ´iyd kimkumbushe pindi watu watapokusanyika katika uwanja mmoja mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Ataona namna ya kutofautiana na kushindana kiubora katika mkusanyiko huu, jambo ambalo litamkumbusha kutofuatiana na kutofautiana kiubora huko Aakhirah. Allaah (Ta´ala) amesema:

انظُرْ كَيْفَ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَى بَعْضٍ وَلَلآخِرَةُ أَكْبَرُ دَرَجَاتٍ وَأَكْبَرُ تَفْضِيلاً

”Angalia vipi tulivyowafadhili baadhi yao kuliko wenginewe. Na hakika Aakhirah ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi.”[1]

Afurahie neema za Allaah kukiwemo kufikiwa na Ramadhaan, kutekeleza zile ´ibaadah zilizomsahilikia kama vile swalah, swawm, usomaji wa Qur-aan, swadaqah na mambo mengine ya utiifu. Kwani hakika mambo hayo ni kheri kuliko ulimwengu wote na vilivyomo ndani yake:

قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ

“Sema: “Kwa fadhilah za Allaah na kwa rehema Zake, basi kwa hayo wafurahi. Hayo ni kheri kuliko wanayoyakusanya.”[2]

Hakika kufunga Ramadhaan na kusimama kuswali nyusiku zake hali ya kuwa na imani na kutaraji malipo ni miongoni mwa sababu za kusamehewa madhambi. Muumini anafurahi kwa kukamilisha funga, kusimama usiku na kusamehewa madhambi. Muislamu mwenye imani dhaifu anafurahi kwa kukamilisha mfungo kwa sababu anapata kujinasua na swawm ambayo ilikuwa ikimtia uzito na kuumpa dhiki moyo wake – kuna tofauti kubwa kati ya furaha hizo mbili!

[1] 17:21

[2] 10:58

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 226
  • Imechapishwa: 31/03/2024