Swali 104: Unasemaje juu ya wale watu wanaotoka nje ya nchi kulingania ilihali hawajawahi kujifunza elimu? Wanahimiza jambo la kutoka, wanarudiarudia nembo za ajabu na wanadai kuwa ambaye anatoka katika njia ya Allaah basi Allaah atampa ilhamu? Wanadai kuwa elimu sio sharti ya msingi. Hakika unajua kuwa mlinganizi anayetoka nje ya Saudi Arabia hukutana na mapote, dini na maswali. Je, huoni kuwa ni lazima kwa mlinganizi awe na elimu ili kuweza kukabiliana na watu? Hilo khaswa Asia ya Mashariki ambapo wanapiga vita ulinganizi wa Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab.

Jibu. Utokaji wanaokusudia ni Bid´ah ambayo haikufanywa na Salaf[1]. Hata hivyo ni sawa kwa mwanachuoni akatoka kulingania kwa Allaah bila ya kujifungamanisha na kundi lolote zaidi ya Ahl-us-Sunnah au akajifungamanisha na siku arobaini, chini ya hapo au zaidi ya hapo.

Vilevile mlinganizi ni lazima awe na elimu. Haijuzu kwa mtu kulingania kwa Allaah hali ya kuwa ni mjinga:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi…´”[2]

Bi maana kwa elimu. Kwa sababu ni lazima kwa mlinganizi ajue kile anacholingania kwacho katika mambo ya wajibu, yanayopendeza, yaliyoharamishwa na yaliyochukizwa. Anatakiwa kujua ni nini shirki, maasi, kufuru, ufuska na maasi. Anapaswa kujua madhambi na ngazi za ukemeaji.

Utokaji unaomshughulisha mtu na kujifunza elimu ni jambo la batili. Kwa sababu kujifunza elimu ni jambo la lazima na halipatikani isipokuwa kwa kusoma. Halipatikani kwa ilhamu. Haya ni miongoni mwa ukhurafi wa Suufiyyah potofu. Kutenda pasi na elimu ni upotofu. Kuwa na matumaini ya kupata elimu pasi na kusoma ni udanganyifu.

[1] ´Allaamah ´Abdur-Razzaaq bin ´Afiyfiy amesema:

”Uhakika wa mambo ni kwamba Jamaa´at-ut-Tabliygh ni wazushi wapindaji walioshikana na amri za Qaadiriyyah na mifumo mingine. Kutoka kwao sio katika njia ya Allaah, bali ni katika njia ya Ilyaas. Hawalingii katika Qur-aan na Sunnah. Wanalingania kwa Shaykh wao Ilyaas.

Ama kutoka kwa kunuia kulingania kwa Allaah ni katika jihaad katika njia ya Allaah. Na si utokaji huu wa Jamaa´at-ut-Tabliygh. Nawajua Jamaa´at-ut-Tabliygh tangu zama za kale. Ni wazushi popote wanapokuwa; Misri, Israel, Amerika au Saudi Arabia. Wote wamefungamana na Shaykh wao Ilyaas.” (Fataawaa ash-Shaykh ´Abdur-Razzaaq ´Afiyfiy (1/174))

[2] 12:108

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 245-247
  • Imechapishwa: 13/08/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy