103. Kuna sababu gani ya kuyanasibisha makundi yaliyopo leo hii na Uislamu?

Swali 103: Kuna sababu gani ya kuyanasibisha makundi yaliyopo leo hii na Uislamu?

Jibu: Makundi ni mapote yaliyopo kila zama na jambo hili si la ajabu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mayahudi wamegawanyika makundi sabini na moja. Manaswara wamegawanyika makundi sabini na mbili.  Na Ummah wangu utagawanyika katika mapote sabini na mbili. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: ”Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Ni lile linalofuata yale ninayofuata mii hii leo na Maswahabah zangu.”[1]

Kuwepo kwa makundi na mapote si jambo la kushangaza. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika yule katika nyinyi atakayeishi kipindi kirefu basi atakuja kuona tofauti nyingi.”[2]

Lakini kundi pekee ambalo ni wajibu kujiunga nalo, kufuata mwongozo wake na kuwa nalo ni Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mayahudi wamegawanyika makundi sabini na moja. Manaswara wamegawanyika makundi sabini na mbili.  Na Ummah wangu utagawanyika katika mapote sabini na mbili. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: ”Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Ni lile linalofuata yale ninayofuata mii hii leo na Maswahabah zangu.”[3]

Hiki ndio kigezo. Makundi yote yanapaswa kukaguliwa kupitia ´Aqiydah aliyokuwa nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake[4]. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia mwanzoni ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[5]

Hawa ndio Mkusanyiko na ni kundi moja tu ambalo halina mipasuko wala migawanyiko[6]. Daima limekuwa hivo mpaka hii leo:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

”Na wale waliokuja baada yao wanasema: ”Ee Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu!”[7]

Kundi hili lipo kuanzia wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka kusimama kwa Qiyaamah. Nao ni Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah[8]. Makundi mengine yote yanayoenda kinyume nao yanatakiwa kupuuzwa ingawa yatajinasibisha na Uislamu, ulinganizi au kitu kingine. Makundi yote yanayoenda kinyume na Mkusanyiko, ambayo kiongozi wake alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ni katika mapote yaliyopinda na yanayogawanyisha ambayo haifai kwetu kujiunga wala kujinasibisha nayo. Haitakiwi kwetu kujinasibisha isipokuwa na Ahl-us-Sunnah wapwekeshaji:

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ

“Tuongoze njia iliyonyooka; njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea!”[9]

Amewataja watu hawa walioneemeshwa pale aliposema:

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha – Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa na tangamano kama hili!”[10]

Kundi pekee linalozingatiwa ni lile ambalo limejenga mfumo wake juu ya Qur-aan na Sunnah na kufanyia kazi maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hakika yule katika nyinyi atakayeishi kipindi kirefu basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza. Ziumeni kwa magego yenu. Na nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotofu.”[11]

Makundi mengine yote yanatakiwa kupuuzwa. Bali ni makundi yaliyopinda, kila mmoja kutegemea na umbali au ukaribu wake na haki. Hata hivyo yote yako chini ya matishio ya kuingia Motoni.

[1] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

[2] Ahmad (4/126).

[3] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

[4] Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Makundi yote yanadai kuwafuata Salaf pasi na kufanyia kazi yale waliyokuwemo Salaf.” (Fataawaa al-´Ulamaa’ al-Kibaar, uk. 98)

[5] 09:100

[6] ´Allaamah Bakr Abu Zayd (Rahimahu Allaah) amesema:

”Mkusanyiko wa waislamu kwa mujibu wa mfumo wa kinabii haukubaliani na migawanyiko wala kutawanyika. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake walikuwa wakilingania kwa ajili ya kuunda mkusanyiko wa Kiislamu wenye kuita umoja kama wa waislamu, kundi lililonusuriwa, kundi lililookoka na Salaf. Watu hawa ni wale wenye kufuata yale aliyokuwa akifuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake. Ameamrisha kulazimiana nao na amekemea kutengana nao, kama alivokataza kugawanyika kati yao.” (Hukm-ul-Intimaa’, uk. 60)

[7] 59:10

[8] ´Allaamah Bakr Abu Zayd (Rahimahu Allaah) amesema:

”Waislamu hawana kingine zaidi ya Qur-aan na Sunnah na kulingania katika viwili hivyo kutokana na mfumo wa kinabii. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ni lile linalofuata yale ninayofuata mii hii leo na Maswahabah zangu.”

Ni wale ambao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaita ”Mkusanyiko”. Wakati alipotaja mapote potevu akawaeleza kuwa ni Kundi lililonusuriwa na Kundi lililookoka. Wanajinasibisha na Sunnah na njia yake na Salaf. Wakati yalipozuka mapote ikaitwa ´Aqiydah yao kuwa ni ya ”Salafiy” na ”Salafiyyah”.” (Hukm-ul-Intimaa’, uk. 112-113)

[9] 1:6-7

[10] 4:69

[11] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 242-245
  • Imechapishwa: 13/08/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy