Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:
Isitoshe watu hawa wako sampuli mbili juu ya mada hii. Wengi wao wanaona kuwa kila ambacho kinakataliwa na akili basi kinatakiwa kutupiliwa mbali. Wengine wanaona kuchukua msimamo wa kusimama na wanamaanisha kuwa kila ambacho hakikubaliwi na akili basi kinatakiwa kukanushwa na wanafanya ndio mahali pa kuanzia wakati wa kutofautiana.
MAELEZO
Mapote haya potofu yamegawanyika makundi mawili. Moja wapo linategemea akili. Yale yanayothibitishwa na akili zenu, basi yathibitisheni juu ya Allaah. Na yale yanayokanushwa na akili zenu, basi yakanusheni juu ya Allaah. Hakuna kurejea katika Qur-aan na Sunnah, kwa sababu havibainishi haki.
Kundi lingine linamaanisha yale yanayothibitishwa na akili zenu, basi yathibitisheni juu ya Allaah. Na yale yanayokanushwa na akili zenu, basi wachukue msimamo wa kusimama juu ya Allaah. Kwa msemo mwingine wabaki katika mkanganyo. Ni kama kwamba Allaah (´Azza wa Jall) amewaacha katika hali ya kudangana na kutochukua msimamo wowote hawajui ni wapi ilipo haki. Hivi kweli inamstahikia Allaah kuwaacha waja Wake katika hali ya kuchanganyikiwa pasi na kujua ni wapi ilipo haki? Allaah ametakasika kutokana na hilo. Allaah (Subhaanah) amesema:
فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَن تَبِعَ هُدَايَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ
“Pale ambapo uongofu utakufikieni kutoka kwangu, yeyote atakayefuata uongofu Wangu hakutakuwa na khofu juu yao wala hawatahuzunika. Na wale waliokufuru na wakakadhibisha Aayah Zetu, hao ni watu wa Motoni, wao humo ni wenye kudumu.”[1]
Allaah ameturejesha katika uongofu ambao ameuteremsha kwa Mitume Yake. Yale yanayohusiana na Allaah, majina na sifa Zake hayawezi kutambuliwa isipokuwa tu kwa njia ya Wahy. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:
يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا
“Anajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na hawawezi kumzunguka kwa kumtambua.”[2]
فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ
“Basi msimpigie mifano Allaah, kwani hakika Allaah anajua nanyi hamjui.”[3]
Hakusemwi juu ya Allaah, majina na sifa Zake isipokuwa kwa dalili kutoka katika Wahy unaoteremshwa kutoka kwa Allaah. Kwani Allaah ndiye anayejijua zaidi kuliko wanavyomtambua viumbe Wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye kiumbe anayemtambua Allaah (´Azza wa Jall) zaidi, kwa sababu Allaah ndiye kamtumiliza na akamteremshia Kitabu ili awabainishie nacho watu. Kwa hivyo marejeo ni Qur-aan na Sunnah. Vivyo hivyo mambo mengine yote yaliyofichikana kuhusiana na mambo yaliyopita na yanayokuja huko mbele; hatuzungumzii juu yake pasi na dalili kutoka ndani ya Qur-aan na Sunnah. Hatuthibitishi wala kukanusha kwa mujibu wa akili na fikira zetu, kwa sababu mambo hayo hayatambuliwi na akili wala fahamu zetu. Ni mambo yanayotambulika tu kupitia njia ya Wahy unaoteremshwa kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na yale yaliyofikishwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hii ndio kanuni juu ya mambo yaliyofichikana; hayazungumziwi isipokuwa kwa njia ya Wahy.
[1] 2:38-39
[2] 20:110
[3] 16:74
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 144-146
- Imechapishwa: 02/09/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)