Hivyo basi ni wajibu kwa mahujaji wa Nyumba ya Allaah kutimiza masharti haya ya kupata msamaha huu mkubwa, kwa namna ya kushikamana na utiifu wa Allaah, kulinda Hajj yao dhidi ya mambo yaliyoharamishwa kama vile matusi, matusi na jimaa na mabishano. Aidha wajichunge makosa ambayo watu wengi huyadharau katika zama zetu, kwani maasi yameharamishwa nyakati zote, lakini yamekatazwa zaidi katika Hajj kwa sababu ya heshima ya wakati na mahali na pia kwa sababu ya utukufu wa ´ibaadah hiyo. Mwenye kuhiji huanza kwa kuingia katika hali ya Ihraam na heshima huongezeka kwa kuingia katika Haram na huongezeka zaidi kwa kutekeleza matendo ya Hajj. Hivyo basi ni lazima awe katika hali bora zaidi ya utiifu na heshima.

Ni lazima kwa anayekusudia kuhiji ajifunze hukumu za Hajj na namna ya kutekeleza ´ibaadah hiyo. Kwa mfano atambue namna ya kuingia Ihraam, jinsi ya kutufu, namna ya kufanya Sa´y na hivyo hivyo ´ibaadah nyingine zote , kwa sababu masharti ya kukubaliwa kwa matendo ni pamoja na:

1 – Iwe ni kwa ajili ya Allaah peke Yake.

2 – Iwe imefanywa kwa mujibu wa Shari´ah Yake kama iliyotajwa ndani ya Qur-aan au kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Hili ni ili muislamu amwabudu Mola Wake elimu na uongofu na pia amfuate Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Chukueni namna ya kutekeleza ´ibaadah zenu za Haj kutoka kwangu.”[1]

Ameipokea Muslim.

Njia ya kufanikisha hilo ni mtu awaulize wanazuoni ni namna gani ya kufanya ´ibaadah ya Hajj, asome vitabu vya ´ibaadah ya Hajj – akiwa ni miongoni mwa wanaosoma na kufahamu – au aongozane na kundi ambalo ndani yake kuna mwanafunzi wa elimu ya dini ambaye anaweza kumwelekeza.

Watu wengine hukosea katika kutekeleza Hajj kama vile namna ya kufanya Ihraam, namna ya kufanya Twawaaf, Sa´y na mengineyo, kutokana na mambo yafuatayo:

1 – Kutojua hukumu za ´ibaadah ya Hajj.

2 – Kutowauliza wanazuoni wanaoaminika kwa elimu na uchaji wao.

3 – Kumuuliza mtu asiye mwanachuoni.

4 – Baadhi ya watu wanawafuata wengine kichwa mchunga.

[1] Muslim (1297).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 10/05/2025