Ibn ´Arabiy ni mwenye kuonelea kuwa washirikina wote na waabudu masanamu kwamba wako katika haki, kwa sababu kwa mujibu wake Allaah ni kila kitu kilichopo. Kwa hivyo ina maana ya kwamba yule anayeabudu sanamu, jiwe, mti, mwanaadamu, nyota, amemuabudu Allaah. Anasema kuhusiana na hili:

“Mtu mwenye uelewa wa ukamilifu, ni yule anayeona kila kinachoabudiwa chenye kujionyesha kwa haki kikaabudiwa. Pasina kujali sawa ikiwa ni mwamba, mti, mnyama, mwanaadamu, nyota au Malaika, wanaviita vyote hivyo kuwa ni Allaah pamoja na majina yake maalum.”[1]

Ibn ´Arabiy anaonelea kuwa ´ibaadah zao ni sahihi, kwa kuwa vyote hivo wanavyoviabudu, si vingine isipokuwa ni Yeye Mola ambaye amejionyesha kwa sura ya mtu, mti au jiwe.

Ndugu! Ikiwa Swabaaiyyah walikuwa makafiri kwa ajili ya kuabudu nyota, ikiwa mayahudi walikuwa makafiri kwa ajili ya kuabudu ndama, ikiwa wakristo walikuwa makafiri kwa ajili ya kumuabudu ´Iysaa na ikiwa Quraysh walikuwa makafiri kwa ajili ya kuabudu masanamu… vipi yule anayeita katika kuviabudia vitu vyote hivi asiwe ni kafiri?

Vilevile Ibn ´Arabiy anakubaliana na kwamba dini zote ni dini moja na kuwa yuko tayari kupokea makundi na dini zote. Anasema katika kitabu chake “Dhakhaair-ul-A´laaq Sharh Tarjumaan-il-Ashwaaq”:

“Mpaka hivi leo nilikuwa namkataza swahibu wangu ikiwa hafuati dini yangu. Lakini roho yangu imebadilika na inafuata misimamo yote. Inafanya kazi na wapenzi wa furaha na vyama vya watawa. Nyumba ya waabudu masanamu, Ka´bah Twaaif, vibao vya Tawraat na msahafu wa Qur-aan. Ninaamini dini ya upendo, popote inapoelekea. Dini zote ni dini na madhehebu yangu.”[2]

Vilevile Ibn ´Arabiy alikuwa akiwatahadharisha wafuasi wake kuamini dini moja tu na kukanusha zingine. Amesema katika “al-Fusuusw”:

“Ole wako na kuamini dini moja tu na kukanusha zingine zote, jambo ambalo linapelekea kukosa kheri nyingi. Bali utakuja kukosa elimu juu ya suala analofuata. Badala yake unatakiwa kuwa tayari kuzikubali imani zote. Hili ni kwa sababu Allaah ni Mwenye wasaa na Mkubwa zaidi kuliko kukomeka na imani moja tu. Zote ni zenye kupatia na kila mwenye kupatia atalipwa, kila mwenye kulipwa ni mwenye kufaulu na kila mwenye kufaulu ni mwenye kuridhiwa.”[3]

Kwa ajili hiyo Ibn ´Arabiy ameeleza kwamba Fir´awn amesema wakati wa Muusa aliokolewa. Amewekea taaliki Kauli ya Allaah (Ta´ala) pale aliposema:

قُرَّتُ عَيْنٍ لِّي وَلَكَ

“Kiburudisho cha macho kwangu na kwako.” ( al-Qaswasw 28:09)

 “Kupitia hilo akapata kiburudisho cha macho – yaani mke wa Fir´awn – kutokana na ukamilifu aliopewa, wakati kiburudisho cha Fir´awn ilikuwa imani Aliyompa Allaah wakati alipozama. Hivyo Akaichukua roho yake ikiwa ni safi na yenye kutwaharika, iliyotakasika na uchafu wote.”[4]

Anamhukumu Fir´awn waziwazi kwamba alikuwa muumini, jambo ambalo linaenda kinyume na dalili ya Qur-aan. Miongoni mwazo ni Kauli ya Allaah (Ta´ala):

فَأَخَذَهُ اللَّـهُ نَكَالَ الْآخِرَةِ وَالْأُولَىٰ

“Basi Allaah Alimchukuwa kwa adhabu ya mfano wa pekee ya Aakhirah na ya mwanzo [duniani].” (an-Naazi´aat 79:25)

´Abdul-Kariym al-Jiyliy, aliyefariki 830 H, amesema katika kitabu chake “al-Insaan al-Kaamil”, wakati akibainisha ya kwamba ´Aqiydah yake ni kuonelea kuwa dini zote ni moja na sawa:

“Ninaisalimisha nafsi yangu kule ambako matamanio yangu yananisalimisha. Vipi ninaweza kugombana na hukumu inayopendwa? Mara unaniona nikirukuu Msikitini na wakati mwingine unanipata nikiabudu kanisani. Ikiwa mimi ni mwenye kutenda dhambi kwa mujibu wa hukumu ya Shari´ah, basi kwa uhakika wa elimu mimi ni mwenye kutii.”[5]

Kwa ajili hiyo kwa mujibu wa al-Jiyliy hakuna tofauti yoyote baina ya Misikiti na makanisa. Hata kama alikuwa ni mwenye kuasi maamrisho ya Allaah kwa udhahiri wa Shari´ah – kama jinsi anavyodai mwenyewe – basi kwa undani ni mwenye kumtii Allaah kwa kuwa anatii Matakwa ya Allaah.

Soma pia maneno ya Ibn-ul-Faaridhw alipothibitisha kwamba Allaah ni wale viumbe Wake – Ametakasika Allaah kutokamana na hayo. Anasema:

“Ninaenda mbele katika uhakika wa ukweli. Ubinaadamu ulikuwa nyuma yangu; uko popote pale ninapoelekea. Sio ajabu kuwa watu wameswali mpaka roho Yangu imeketi na inaswali kwa kunielekea na kunitamani Mimi… “

Ibn-ul-Faaridhw ameandika shairi ambapo ndani yake amemuelezea Allaah kwa dhamira ya kike. Ndugu! Ninazidi kukariri ya kwamba hakuna nafasi ya kutosha ya kutaja imani nyingi za Suufiyyah kama imani inayosema kwamba kila kitu ni Allaah, umoja wa dini ambayo yamesemwa na viongozi wao wakubwa kama kwa mfano Ibn-ul-Faaridhw, al-Jiyliy, Ibn ´Ajiybah, Hasan Ridhwaan, Ibn Bashiysh, ad-Damardaash na wengineo. Anayetaka kuona maneno haya, arejee katika kitabu cha ´Abdur-Rahmaan al-Wakiyl (Rahimahu Allaah) “Haadhihi hiyaa as-Suufiyyah”.

[1] al-Fusuusw (1/195), al-Wakiyl: Haadhihi hiyaa as-Suufiyyah, uk. 38.

[2] al-Wakiyl: Haadhihi hiyaa as-Suufiyyah, uk. 94, na anainasibisha kwa “Dhakhaair-ul-A´laaq, uk. 93.

[3] al-Wakiyl: Haadhihi hiyaa as-Suufiyyah, uk. 94, na anainasibisha kwa “al-Fusuusw”, uk. 191.

[4] al-Wakiyl: Haadhihi hiyaa as-Suufiyyah, uk. 95, na anainasibisha kwa “al-Fusuusw”, uk. 201.

[5] al-Wakiyl: Haadhihi hiyaa as-Suufiyyah, uk. 96, na anainasibisha kwa “al-Fusuusw”, (1/69).

  • Mhusika: Shaykh Muhammad bin Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqiyqat-us-Suufiyyah
  • Imechapishwa: 25/12/2019