10. Haijawahi kutokea kuthibitishwa waungu wawili wanaolingana

Ni jambo lisilowezekana kushirikisha katika uola kwa njia ya kuthibitisha waumbaji wawili na wenye kulingana katika sifa na matendo. Kilichofanywa na baadhi ya washirikina ni kwamba waungu wao wanamiliki baadhi ya uendeshaji katika ulimwengu. Shaytwaan amewachezea akili kwa wao kuwaabudu waungu hawa. Matokeo yake akacheza na watu wa kila karne kwa kiwango cha akili zao. Akawaita kundi kuwaabudu kwa kutumia jina la kuwatukuza maiti ambao walitengeneza masanamu yale kutokana na picha zao. Kwa mfano watu wa Nuuh walifanya hivo. Kundi jengine wakayaabudu masanamu katika sura ya nyota ambazo walidai kwamba zina taathira juu ya ulimwengu. Matokeo yake wakazitengenezea nyumba na walinzi. Wakatofautiana juu ya kuabudu kwao nyota hizi. Miongoni mwao wako walioabudu jua, wengine wakaabudu mwezi na wengine wakaabudu nyota nyenginezo mpaka wakazijengea mahekalu; kila nyota ikawa na hekalu lake maalum. Wengine wakaabudu moto ambao ni majusi. Wengine wakaabudu ng´ombe kama inavyofanywa India. Baadhi wakawaabudu Malaika. Wengine wakaabudu miti na mawe. Baadhi wakayaabudu makaburi. Yote haya ni kwa sababu watu hawa wanafikiria kwamba vitu hivi vina kitu katika sifa maalum za uola. Wako ambao wanasema kwamba masanamu haya yanawakilisha vitu vilivyofichikana. Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Msingi wa kuwekwa sanamu ni kuweka shakili ya kile kinachoabudiwa kisichoonekana. Hivyo ndipo wakaliweka sanamu kwa shakili, sifa na sura yake ili liwe naibu wake na lije kusimama mahala pake. Vinginevyo ni jambo linalotambulika kwamba haingii akilini kwamba mtu atachonga gogo au jiwe kwa mkono wake kisha aamini kuwa ndiye mungu wake… “[1]

Ni kama ambavyo waabudu makaburi – tangu hapo kale mpaka hii leo – wanadai kwamba wale maiti watawaombea na watawakalia kati na kati mbele ya Allaah katika kutatua haja zao na wanasema:

مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie.”[2]

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[3]

Ni kama ambavyo baadhi ya washirikina wa kiarabu na manaswara wamefikiria juu ya waungu wao kwamba ni watoto wa Allaah. Washirikina wa kiarabu waliwaabudu Malaika kutokana na kwamba ni wasichana wa Allaah. Manaswara wakamwabudu al-Masiyh (´alayhis-Salaam) kutegemea ya kwamba ni mwana wa Allaah.

[1] Ighaathat-ul-Lahfaan (02/224).

[2] 39:03

[3] 10:18

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 29/01/2020