10. Hadiyth ”Unafikiriaje wawili ambao Allaah ndiye watatu wao?”

Hadiyth ya tano

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ٌ

”Naye Yu pamoja nanyi popote mlipo.”[1]

مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ

“Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao.”[2]

43 – Abul-´Abbaas Ahmad bin ´Abdil-Hamiyd al-Maqdisiy ametukhabarisha: Abu Naswr Muusa bin ´Abdil-Qaadir al-Jiyliy ametuhadithia mwaka wa 618: ´Abdul-Awwal bin ´Iysaa as-Sijziy ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan bin Muhammad ad-Daawuudiy ametuhadithia: ´Abdullaah bin Hammuuyah as-Sarkhasiy ametuhadithia: Ibraahiym bin Khuzaym ash-Shaashiy ametuhadithia mwaka wa 316: ´Abd bin Humayd ametuhadithia: Habbaan bin Bilaal ametukhabarisha: Hammaam ametuhadithia: Thaabit ametuhadithia: Anas ametuhadithia ya kwamba Abu Bakr as-Swiddiyq alisema akumwambia:

”Wakati tulipokuwa ndani ya pango nilitazama miguu ya washirikina. Nikasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Lau mmoja wao angelitazama miguu yake kwa chini basi angelituona.” Akasema: ”Ee Abu Bakr! Unafikiriaje wawili ambao Allaah ndiye watatu wao?”[3]

Ameipokea Muslim kupitia kwa ´Abd bin Humayd.

44 – Watu wa tafsiri, akiwemo adh-Dhwahhaak, wamesema kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ

“Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao.”[4]

”Yuko juu ya ´Arshi na utambuzi Wake uko pamoja nao.”

45 – Maalik amesema:

”Allaah yuko juu ya mbingu na ujuzi Wake uko kila mahali.”

46 – Sufyaan amesema kuhusu maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ٌ

”Naye Yu pamoja nanyi popote mlipo.”

”Bi maana ujuzi Wake.”[5]

47 – Muqaatil  bin Hayyaan amesema maneno Yake Allaah (Ta´ala):

مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ

“Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao.”

”Yuko (Ta´ala) juu ya ´Arshi na ujuzi Wake uko pamoja nao.”[6]

Amesema (Rahimahu Allaah) kuhusu ukaribu wa Allaah:

”Bi maana kwa ujuzi Wake na wakati huohuo Yuko juu ya ´Arshi Yake.”[7]

48 – Wakati Nu´aym bin Hammaad, mwalimu wake na al-Bukhaariy, alipoulizwa kuhusu maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ٌ

”Naye Yu pamoja nanyi popote mlipo.”[8]

akasema:

”Maana yake ni kwamba hakuna chochote kile kinachojficha Kwake.”

[1] 57:4

[2] 58:7

[3] Muslim (2381).

[4] 58:7

[5] Kitaab-us-Sunnah, uk. 187-189

[6] Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah (3/387-402).

[7] al-Asmaa’ was-Swifaat, uk. 542, ya al-Bayhaqiy.

[8] 57:4

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 61-64
  • Imechapishwa: 02/06/2024