1. Virusi vya corona – Kila kitu kinapitika kwa makadirio ya Allaah

Siku hizi katika vikao vingi vya watu wanazungumzia maradhi wanayoyaogopa na kuchelea juu ya kuenea kwake na kuwapatwa. Wapo ambao wanazungumza kwa utani na kufanya mzaha, wengine hali ya kubainisha na kuwatakia kheri wengine au malengo mengine. Lililo la wajibu kwa muislamu katika kila hali, wakati, janga na kila msiba ni kushikamana barabara na Allaah (Jalla wa ´Alaa) na kuwe kuyazungumza na kuyatibu kwake kumejengeka juu ya msingi wa Kishari´ah na kumcha Allaah. Hapa chini nitaorodhesha nukta sita juu ya maudhui haya ambayo ni muhimu sana katika maisha ya watu hii leo:

1- Lililo la wajibu kwa kila muislamu awe katika hali zake zote ni mwenye kushikamana barabara na Allaah, hali ya kumtegemea na kuamini kwamba mambo yote yako mikononi Mwake:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hausibu msiba wowote [kukupateni] isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Yeyote   anayemuamini Allaah, basi huuongoza moyo wake. – Allaah kwa kila kitu ni mjuzi.”[1]

Mambo yote yako mikononi mwa Allaah; anachotakiwa Allaah, kinakuwa, na kile asichotaka, hakiwi – hakuna mwengine anayelinda isipokuwa Allaah:

قُلْ مَن ذَا الَّذِي يَعْصِمُكُم مِّنَ اللَّـهِ إِنْ أَرَادَ بِكُمْ سُوءًا أَوْ أَرَادَ بِكُمْ رَحْمَةً ۚ وَلَا يَجِدُونَ لَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا

“Sema: “Ni nani ambaye anaweza kukulindeni kutokamana na Allaah kama akikutakieni uovu au akikutakieni rehema?” – na wala hawatopata badala ya Allaah mlinzi na wala mnusuraji.”[2]

قُلْ أَفَرَأَيْتُم مَّا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ إِنْ أَرَادَنِيَ اللَّـهُ بِضُرٍّ هَلْ هُنَّ كَاشِفَاتُ ضُرِّهِ أَوْ أَرَادَنِي بِرَحْمَةٍ هَلْ هُنَّ مُمْسِكَاتُ رَحْمَتِهِ

“Sema: “Je, mnaonaje wale mnaowaomba badala ya Allaah ikiwa Allaah atanikusudia dhara, je, wao wataweza kuondosha dhara Yake au akinikusudia rehema, je, wao wataweza kuzuia rehema Zake?”[3]

مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Rehema yoyote anayoifungua Allaah kwa watu, basi hakuna awezaye kuizuia, na anayoizuia, basi hakuna wa kuipeleka baada Yake – Naye ni Mwenye nguvu zisizoshindikana, Mwenye hekima.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ee kijana! Hakika mimi nitakufunza baadhi ya maneno. Muhifadhi Allaah Naye atakuhifadhi. Muhifadhi Allaah utamkuta mbele Yako. Ukiuliza basi muulize Allaah. Ukiomba basi mwombe Allaah. Jua kwamba endapo Ummah wote utakusanyika juu ya kukunufaisha kwa kitu, basi hawawezi kukunufaisha isipokuwa kwa kitu alichokuandikia Allaah. Na endapo utakusanyika juu ya kukudhuru kwa kitu, basi hawawezi kukudhuru isipokuwa kwa kitu alichokiandika dhidi yako. Kalamu zimenyanyuliwa na madaktari yamekauka.”[5]

”Allaah aliandika makadirio ya viumbe miaka 50.000 kabla ya kuumba mbingu na ardhi na ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.”[6]

”Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: ”Andika!” Ikasema: ”Mola wangu! Niandike nini?” Akasema: ”Andika yale yote yatakuweko mpaka siku ya Qiyaamah.”[7]

Ni lazima kwa kila muislamu kuyategemeza mambo na matumaini yake kwa Allaah hali ya kuwa ni mwenye kumtaraji na ni mwenye kumtegemea. Asitaraji kuwa kusalimika na kupona kwake kunatokana na mwengine asiyekuwa Mola Wake (Tabaarak wa Ta´ala). Majanga na misiba mbalimbali imzidishie kushikamana barabara na Allaah:

وَمَن يَعْتَصِم بِاللَّـهِ فَقَدْ هُدِيَ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

“Atakayeshikamana barabara na Allaah, basi hakika ameongozwa kuelekea njia iliyonyooka.”[8]

[1] 64:11

[2] 33:17

[3] 39:38

[4] 35:02

[5] Ahmad (1/307) na at-Tirmidhiy (2516) aliyesema: ”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

[6] Muslim (2653).

[7] Abu Daawuud (4700) na at-Tirmidhiy (2155). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (2017).

[8] 03:101

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://ar.islamway.net/article/80439/%D9%81%D9%8A%D8%B1%D9%88%D8%B3-%D9%83%D9%88%D8%B1%D9%88%D9%86%D8%A7-%D8%A7%D9%84%D8%AC%D8%AF%D9%8A%D8%AF-%D9%81%D9%8A%D8%B1%D9%88%D8%B3-%D8%A7%D9%84%D8%B5%D9%8A%D9%86
  • Imechapishwa: 08/03/2020