Mtu anatakiwa kujizoeza swawm za Sunnah. Lililo bora ni mtu kujizoeza kufunga siku tatu kila mwezi. Imepokelewa ya kwamba ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alikuwa ameiahidi nafsi yake kufunga kila siku na kuswali usiku mzima. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofikiwa na khabari hizo akamwendea na kumwambia:

“Wewe ndiye umesema hivo?” Akasema: “Ndio, na sikukusudia jengine isipokuwa kheri.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Usifanye hivo. Iwapo utafanya hivo macho yatashuka na nafsi itachoka. Nafsi yako kwako ina haki, jicho lako kwako lina haki, mke wako kwako ana haki na Mola Wako kwako ana haki. Hivyo mpe kila mwenye haki haki yake.”[1]

Salaf wengi walikuwa wakipupia ´ibaadah na wakiitilia umuhimu mkubwa. Kuna mtu alikuwa akikesha usiku mzima na akiswali. Pamoja na kuwa mkewe anataka kuutumia usiku akiwa na yeye lakini mwanaume huyo akikataa. Mwanamke yule akamwendea ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) na kumwambia: “Mume wangu anafunga mchana na anasimama usiku.” Akasema: “Ni mume mzuri aliyoje ulienae.” Mwanamke huyo alisema hivo kwa haya. Wakati huo huo kulikuwepo mwanaume mwenye busara mbele ya ´Umar ambaye akasema: “Ee kiongozi wa waumini. Mwanamke huyu amekujia ili kumshtaki mumewe.” Akamwita na kumwambia: “Nenda na umwite mume wako.” Mwanamke yule akaenda na akarudi na mumewe. ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) akasema kumwambia yule mwanaume: “Hukumu baina yao. Wewe ndiye ulijua kupitia maneno yake ambacho sikukijua mimi. Lazima uwahukumu.” Mwanaume yule akamwambia: “Mke wako anakushtaki kuwa unasimama usiku kucha, unafunga mchana mzima na unamhama kitandani.” Mtu yule akasema: “Ndio. Nataka kumuabudu Mola Wangu.” Mwanaume yule akamuuliza: “Je, una mke mwingine mbali na huyu?” Akasema: “Hapana.” Mwanaume yule akasema: “Allaah amekuruhusu wewe kuoa wake wane. Lau ungelikuwa na wake wane basi huyu angelikuwa na haki ya moja ya nyusiku nne. Una haki ya kuabudu nyusiku tatu. Usiku wa nne ni lazima uutumie ukiwa na mkeo.”[2]

Makusudio ya haya yote ni kwamba zile karne za kwanza watu walikuwa wakipenda ´ibaadah tofauti na hivi sasa watu wameipa mgongo ´ibaadah. Unataka kutoka kwa watu wafanye mambo ya wajibu, lakini hata hayo pia watu wengi wanayapuuza. Ee mja wa Allaah! Chunga usije kujisababishia ghadhabu za Allaah. Ukimuomba Allaah (Subhanahu wa Ta´ala) uongofu na ukatafuta radhi  Zake, atakuongoza na kukufanya kuwa katika wachaji Allaah.

[1] al-Bukhaariy (1979) na Muslim (1159).

[2] al-Qurtwubiy amemnasibishia kisa hiki az-Zubayr bin Bakkaar.Tazama ”al-Jaami´ li Ahkaam-il-Qur-aan” (5/19).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Istiqbaal Shahri Ramadhwaan, uk. 44-47
  • Imechapishwa: 09/06/2017